***************************************
Na Farida Saidy,Morogoro.
Jumuiya ya vijana kutoka Raleigh Tanzania imejipanga kuongeza matumizi ya nishati endelevu kwa vijana milioni 10 na tasisi 20 ifikapo juni 2022 ili kukabiliana na upotevu wa misitu unaopelekea uharibifu wa mazingira.
Hayo yamesemwa na katibu wa jumuiya hiyo Bwana Elibariki Simon wakati wa uzinduzi wa kampeni ya KESHO TUTACHELEWA iliyofanyika Mkoani Morogoro, ambapo amesema hadi kufikia mwaka 2022 vijana milioni 10 watakuwa wamejiunga na harakati ya Raleigh Tanzania kupitia kampeni hiyo.
Amesema ili kufikia malengo hayo Raleigh wanashirikiana na mashirika mbalimbali ikiwemo wadau na sekta za serikali za mazingira wakiwemo wakala wa misitu Tanzania (TFS) na mashirika mengine ili kuongeza tija katika zoezi hilo.
Hata hivyo amesema kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya maliasili na utalii Tanzania inapoteza hekta laki 3 – 4 za misitu kila mwaka, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa dunia.
Aidha ameongeza kuwa swala la uvunaji wa mbao, mkaa na bidahaa nyingine za misitu zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, ambapo kati ya mwaka 2001 na 2015 hekta milioni 1.8 za misitu zimepotea kwa ripoti ya Umoja wa Mataifa(UN).
Kwa upande wake mratibu wa mradi wa jumuiya ya umoja wa vijana wa Raleigh Tanzania Bwana Gerald Tupa, amesema jumuiya hiyo inazaidi ya vijana 15000 kutoka mikoa yote ya Tanzania.
Aidha amesema katika mwendelezo wa kampeni ya upandaji miti jumla ya miti 40,000 imepandwa katika mwaka 2016 hadi 2017 katika mikoa ya morogoro,arusha na mwanza.
Awali akizindua kampeni hiyo afisa mazingira Manispaa ya Morogoro Alex Romani amewataka wadau wengine wa mazingira kujitokeza kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.