Home Biashara MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA WA MAHAKAMA WAPIGWA MSASA

MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA WA MAHAKAMA WAPIGWA MSASA

0

Mkuu wa Chuo Dkt. Paul F. Kihwelo  akifungua Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yanaoyofanyika katika ukumbi wa Chipeta uliopo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Dar es Salaam

Baadhi ya Washiriki katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Sehemu ya washiriki wakifatilia Mafunzo

Baadhi ya Washiriki katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

Sehemu ya washiriki wakifatilia Mafunzo

…………………………………..

Na: Rosena Suka IJA

Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania wanashiriki katika mafunzo ya wiki mbili yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama  Lushoto.  Akifungua Mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Chipeta uliopo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania  amewataka Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa na mijadala huru itakayosaidia kuboresha utendaji kazi wao ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. 

Mafunzo haya  yamekusanya zaidi ya washiriki 40 kutoka katika sekta mbalimbali za umma na  binafsi. Akielezea lengo kuu la mafunzo  hayo Mhe. Dkt. Kihwelo amesema endapo Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama watalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi ni dhahiri kuwa Mahakama ya Tanzania pia itakuwa imelalamikiwa kwa kuwa watu hao hufanya kazi na Mahakama.

Kuanzishwa kwa mafunzo ya Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea katika muhimili wa Mahakama. Hili linafanyika ili kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi. Inatazamiwa kuwa kwa kupata mafunzo haya Madalali na Wasambaza Nyaraka watafanya kazi kwa kufuata kanuni zilizopo.

Dkt. Kihwelo aliendelea kwa kusema kuwa lengo lingine la mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa Mahakama ya Tanzania inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka wenye mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi.

Mratibu wa mafunzo hayo Bi Hamisa Mwenegoha alipokuwa  akimkaribisha  Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul Kihwelo  alisema mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya sita kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama ili kuwajengea uwezo na kukuza taswira nzuri ya Mahakama ya Tanzania.

Alisema sheria inaweka masharti kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuhuisha leseni za kufanyia shughuli hizo ili kutimiza matakwa ya sheria inayoongoza shughuli zao. Pamoja na mambo mengine, sheria imeweka vigezo vya mtu mwenye kufanya shughuli hizo ambapo moja ya vigezo hivyo ni kupatiwa mafunzo ya umahiri kutoka chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Mafunzo mengine ya aina hiyo yatatolewa katika vipindi tofauti tofauti kwa lengo la kumpa fursa mtu yeyote mwenye vigezo stahiki kupatiwa mafunzo maalum yatakayomwezesha kupata cheti cha umahiri katika udalali na usambazaji nyaraka za Mahakama Pamoja na kuifanya kazi hiyo kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kisheria zilizopo.