**********************************
Wafanyabiashara wa mbao mkoani Dar es Salaam waiomba Serikali kuweka utaratibu rafiki utakaolahisisha ustawi wa biashara ya mazao ya misitu hususan mbao na samani ili kuiwezesha serikali kupata mapato kupitia kodi huku wafanyabishara nao wakinufaika na shughuli hiyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Samani Keko, Pantaleo Valantine Banzi baada ya umoja wao kutakiwa kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa malighafi ya miti, mitaji, na masoko ya mbao na samani inayotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS katika mkutano maalumu wa wafanyabishara hao na TFS uliofanyika jijini Dar es salaam jana.
“Sisi wafanyabiashara wa samani tumekuwa tukiangaika sana kupata malighafi za mazao ya misitu, watu wa kati wanatuumiza lakini kupitia kikao hiki tumeona nia njema ya serikali kutukomboa!
“Naibu Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Mohamed Kilongo ametueleza jinsi gani TFS imejipanga kuhakikisha sisi wafanyabiashara tunawekewa mazingira wezeshi katika upatikanaji wa malighafi mbao ili tuweze kufanya shughuli zetu kwa ufanisi na tija huku tukitoa mchango stahiki katika maendeleo ya nchi, lakini tuiombe Serikali sasa iutambue rasmi mti wa misaji (teak) kama mbao ngumu pindi inapotangaza zabuni zake,“ anasema Valentine.
Kwa upande wake Naibu Kamishna Kilongo anasema Serikali imeshatoa maelekezo mbalimbali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 ambapo moja ya maelekezo hayo ao kwao ni kuhakikisha waendeleza viwanda vya mazao ya misitu na nyuki vinavyochakata mazao hayo kwa ufanisi na tija.
“Leo tunakutaka katika kikao hiki kama tulivyoelekezwa na viongozi wetu, tunatajka mjue fursa tulizonazo TFS, sasa mmeniambia umoja wenu Keko una wafanyabishara 1826, ni wajibu wetu kuwahudumia, tuwahudumie kwa maana ya kupata mazao bora ya misitu kwa ajili ya kutengeneza samani kwa njia yoyote ile ili kukuza uchumi, jipangeni ili mtumie fursa tulizonazo ili sisi kama Serikali tuweze kuwahudumia,”
“Tunajua mnatumia sana mbao ngumu katika shughuli zenu za kila siku, nataka kuwaambia kwamba mbao za misaji (teak) zina ubora sawa na mbao za mninga na mkongo, na mbao za misaji zinapatikana kwa urahisi katika mashamba yetu njooni tuwape mitaji na mnunue kitu kilicho bora,” alisema Naibu Kamishna Kilongo.
Aidha, Naibu Kamishna Kilongo anasema TFS imeshirikiana na kushirikiana na NMB katika kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakuwa na mitaji itakayowawezesha kuwekeza kwenye viwanda vya kisasa vya misitu pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) watakaosimamia suala la masoko.