*************************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
UPUNGUFU wa saruji uliojitokeza hapa nchini ,ikiwemo mkoa wa Pwani,haujaathiri ujenzi wa miradi mikubwa ya Kitaifa ya kimkakati na ujenzi wa viwanda licha ya mkoa huo kuwa na mahitaji makubwa ya saruji.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo akiwa na uongozi wa wilaya ya Kibaha walipofanya ziara kutembelea wauzaji wakubwa wa saruji kwenye mji wa Kibaha.
Alisema ,mahitaji mkoa wa Pwani ni makubwa kutokana na miradi mikubwa pamoja na ujenzi wa viwanda ambavyo vinajengwa kwa kasi kubwa.
Ndikilo alieleza,kwa muda sasa kumekuwa na upungufu mkubwa wa saruji kwenye mkoa huo kutokana na baadhi ya viwanda kusimamisha uzalishaji na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati hata hivyo upungufu huo haujaathiri ujenzi wa miradi hiyo mikubwa hapa nchini.
“Nimetembelea na kujionea mwenyewe changamoto ya upungufu wa saruji lakini hakuna athari ambazo zimejitokeza kwenye ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na ule wa uzalishaji umeme kule Rufiji wa Nyerere, ujenzi wa reli ya mwendokasi ya (SGR) na ujenzi wa barababara kutoka Jijini Dar es Salaam kuja Kibaha lakini wajenzi wanaendelea na kazi zao,”alisema Ndikilo.
“Kule tumekuta shughuli zinaendelea labda watakuwa wanapata saruji kwa njia nyingine lakini hakuna tatizo la upungufu kwenye ujenzi huo unaoendelea lakini tunaomba viwanda nchini viendelee kuzalisha kwa wingi ili ujenzi usikwame sababu ujenzi unafanyika kwa kiasi kikubwa sana,”alisema Ndikilo.
Alisema , kabla ya saruji kupotea bei ilikuwa wastani wa shilingi 13,500 hadi 14,000, 14,500 hadi 15,000 hata hivyo bei haijabadilika sana kwani kwa sasa ni 14,500, 14,700 na 15,000 tofauti na mikoa mingine au maeneo mengine ambapo wanasema imefikia hadi 20,000 na zaidi.
Moja ya wauzaji Denis Magese ambaye ni ofisa masoko kutoka kampuni ya VGK kanda ya Kibaha alisema kuwa kwa sasa saruji ni upungufu mkubwa ambapo kwa sasa wanadaiwa tani 300 kwa wateja ambao tayari walishalipia lakini kutokana na uhaba huo wanasubiri.
Nae muuzaji wa saruji Rahel Msaki alisema kuwa kwa sasa wanakaribia mwezi mzima hawana saruji na wanapowauliza mawakala wanaowaletea wanasema kuwa huko viwandani wanaambiwa kuna foleni kubwa hivyo wasubiri na hawajui wasubiri kwa muda gani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, amefanya ukaguzi kwa Mawakala na Wauzaji Jumla na Rejareja wa Saruji ,Wilayani Kibaha , Lengo likiwa ni Utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri Mkuu la Kusimamia Udhibiti wa Bei ya Saruji Nchini.