…………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Jitihada za kuanzisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii zinazidi kushika kasi ambapo safari hii Serikali imemtua Mama wa Mihambwe ndoo kichwani.
Wakazi wa kata ya Mihambwe na viunga vyake walikuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama ambapo sasa tatizo limebaki historia na Wananchi kujivunia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama dola Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamejionyesha kwenye ziara aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ya kukagua miradi ya maji iliyopo kata ya Mihambwe ambapo alishiriki tukio la kumtua Mama ndoo kichwani ambapo awali walitumia muda mrefu na umbali mkubwa kusaka maji.
“Tunazidi kujenga historia kwa Serikali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kutatua changamoto za upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini na mijini ambapo sasa maji ni ya uhakika na yapo jiraani na Mwananchi anapoishi. Mradi huu wa maji utaondoa tatizo kwa ngazi zote za vitongoji, vijiji na kata ya Mihambwe. Pongezi kwa wote na rai kwa Wananchi wa Tarafa ya Mihambwe kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kushirikiana na Serikali ambayo ipo kazini kuwatatulia kero zao” alisema Gavana Shilatu.
Akizungumza kwa niaba ya Wanawake na Wananchi Bi Hadija Mkalama alipongeza kwa mradi huo wa maji na kuomba uzidi kuboresha na uwe endelevu.
“Sisi Watu wa Mihambwe hatuamini leo hii tuna maji Safi na salama tena tukiyapata kiurahisi, ni ndoto iliyotimia. Tunamshukuru Rais Magufuli na Serikali yake kwa maendeleo haya.” Alimalizia Bi Hadija.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Afisa Maendeleo kata, Watendaji vijiji pamoja na uongozi wa halmashauri Serikali za Vijiji katika kukagua na kumtua Mama ndoo kichwani.