Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akizungumza jana na wajasiriamali kutoka vikundi 45 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua waliopatiwa mikopo yenye thamani shilingi milioni 290.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua Michael Nyahinga akitoa maelezo ya utangulizi jana kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kwa ajili ya kutoa nasaha zake kwa wajasiriamali kutoka vikundi 45 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua waliopatiwa mikopo yenye thamani shilingi milioni 290.
Baadhi ya wajasiriamali kutoka vikundi 45 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua waliopatiwa mikopo yenye thamani shilingi milioni 290 wakimsikiliza jana Mgeni rasmi wakati wa sherehe fupi ya kupewa mikopo hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Jerry Mwaga akitoa taarifa fupi jana kuhusu wajasiriamali kutoka vikundi 45 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua waliopatiwa mikopo yenye thamani shilingi milioni 290.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akikata utepe ikiwa ni ishara ya kukabidhi pikipiki 30 kwa vikundi vitatu vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua zenye thamani shilingi milioni 72 ikiwa ni sehemu ya mkopo wa thamani ya milioni 290 uliotolewa jana katika vikundi 45.
Mbunge wa Jimbo la Kaliua Alyoce Kwezi akizungumza jana na wajasiriamali kutoka vikundi 45 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua waliopatiwa mikopo yenye thamani shilingi milioni 290.
Picha na Tiganya Vincent
………………………………………………………………………………….
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua imetoa vifaa vya usafiri na mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 290 kwa vikundi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.
Mikopo hiyo imekabidhiwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Philemon Sengati kwa niaba ya uongozi wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Jerry Mwaga alisema kati ya fedha shilingi milioni 156 zimetolewa kwa vikundi 17 vya vijana na shilingi 119 zimetolewa kwa vikundi 23 vya wanawake na shilingi milioni 15 zimetolewa kwa vikundi vitano vya watu wenye ulemavu.
Alisema kati ya fedha zilizotolewa kwa vikundi vya vijana kiasi ya shilingi milioni 72 zimetumika kununua pikipiki 30 ambazo zimetolewa kwa vikundi vya bodaboda toka kata za Ushokola, Usinge na Ichemba.
Mwaga alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imeendelea kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu vilivyosajiliwa.
Alisema kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/15 hadi 2020/21 wameshakopesha jumla ya shilingi bilioni 1.4 kwa vikundi 330.
Mwaga alisema vikundi vya vijana 128 vimekopeshwa jumla ya shilingi 772.4, wanawake vikundi 177 vimekopeshwa milioni 605.3 na vikundi 25 vya watu wenye ulemavu vimekopeshwa shilingi milioni 71.5.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa wanaendelea kufuatilia deni la shilingi bilioni 1 ambazo ni fedha zilizokopeshwa kwa vikundi na bado haijareshwa na wakopeshwaji.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati amezitaka Halmashauri nyingine mfano wa Kaliua katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya vijana , walemavu na Wanawake.
Alivitaka vikundi vilivyokopeshwa kuhakikisha wanazitumia katika malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Sengati aliongeza kuwa fedha walizokopeshwa ni lazima zirejeshwa katika muda uliopangwa kwa ajili ya kuvisaidia vikundi vingine vilivyosajiliwa katika masuala ya maendeleo.
Alisema Kaliua imeweza kutoa mikopo ambayo itayasaidia makundi hayo kujipatia kipato na kujiletea maendeleo yao na Taifa.
Aidha Dkt. Sengati aliutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kuendelea kuvijengea uwezo vikundi viweze kutumia mikopo wanayowapatia kuendesha shughuli zao za maendeleo kisayansi na teknolojia kwa ajili ya kuuza uchumi wa wakazi wake.