Na. Beatrice Sanga
MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 kwa kutwaa ubingwa wa kombe la Baraza la Chama cha Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) baada ya kuifunga Zambia kwa mikwaju ya penati 4-3. Hatua hiyo ilikuja baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo katika fainali zilizomalizika huko nchini Afrika Kusini
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, katika hafla iliyofanyika Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo ameipongeza timu hiyo kwa kupata ubingwa na kueleza kuwa Serikali imefurahishwa na ushindi huo.
Singo amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Michezo imejipanga kuhakikisha timu za Taifa zinafanya vizuri kwa kutoa kipaumbele kwa wachezaji ili waweze kucheza katika hali nzuri na kuendelea kuwapatia ushindi Watanzania
“Timu zetu zitakuwa zinasaidiwa kwa karibu na Serikali kupitia vyama vyote vya michezo na tutahakikisha Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Serikali vinashiriki kikamilifu ili kuhakikisha timu zetu za Taifa zinapata ushindi katika mashindano yote”, amesema Singo
Aidha kamati ya Hamasa ya Taifa Stars iliyoundwa kwa ajili ya kuongoza timu ya taifa kupata ushindi imekabidhi zawadi ya dola za Kimarekani 15,000 kama ilivyokuwa imeahidi kwa timu hiyo ya wanawake chini umri wa miaka 17.
Akikabidhi zawadi hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Mkuu wa kamati hiyo Hersi Saidi ameipongeza timu hiyo na kuahidi kuwa kamati hiyo itaendelea kutoa kipaumbele kwa karibu ili kuhakikisha timu hizo zinapata ushindi.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, nahodha wa timu Irene Kisisi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuthamini soka la wanawake kwa kutoa kipaumbele katika michezo kwa ujumla huku akiwahakikishia Watanzania kwamba timu hiyo itaendelea kufanya vizuri katika michuano inayofuata
“Kwa niaba ya wachezaji wenzangu tunapenda kuishukuru TFF kwa kuthamini soka la wanawake na kutoa sapoti, pia tunapenda kuishukuru Serikali kwa kuona kile ambacho tunafanya na kuweza kutupa sapoti nasi tunaahidi tutaendelea kufanya vizuri”, amesema Irene
MWISHO