Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Yasinta Alute akifungua
mafunzo ya elimu ya utambuzi juu ya mambo mbalimbali kwa wasichana
yanayofadhiliwa na CAMFED, ikiwemo uelewa ya afya ya uzazi, UKIMWI,
Ujasiriamali na namna ya kubaini fursa zinazozunguka jamii na njia bora ya
kuzifikia mkoani Singida jana. Kulia ni Mjumbe wa shirika hilo Paschal
Kichambati, Mkuu wa Miradi Nasikiwa Mwalisu na Mwenyekiti wa CDC Manispaa ya
Singida, Omary Kisuda.
– Mkuu
wa Miradi Nasikiwa Mwalisu akitoa mada kwenye mafunzo hayo.
Mwenyekiti
wa CDC Manispaa ya Singida, Omary Kisuda akizungumza.
Washiriki
kutoka Wilaya za Manyoni na Singida Manispaa wakifuatilia mafunzo hayo.
Mafunzo
yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
Mwenyekiti
wa CAMA wilaya ya Manyoni, Bahati Ismaili akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
Na Godwin Myovela, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la CAMFED limewataka wasichana
mkoani hapa kutobweteka, na badala yake kutazama fursa zinazowazunguka na
kuzigeuza kuwa chanzo cha kuinua kipato katika muktadha chanya wa kuibadili
jamii kimaendeleo.
Imeelezwa stratejia mojawapo itakayowasaidia wasichana
hususani wale waliojifungua katika umri mdogo -ni kuwawezesha kwa kuwajengea
pamoja na mambo mengine, misingi ya kutambua haki ya wao kupata elimu juu ya afya
ya uzazi na UKIMWI.
Akizungumza mkoani hapa wakati wa mafunzo hayo ya kuwawezesha
kujitambua, sambamba na kutambua fursa mbalimbali zinazowazunguka nje ya mfumo
rasmi wa elimu, Mkuu wa Miradi kutoka Camfed, Nasikiwa Mwalisu alisema kama mtoto
wa kike akijilinda na kuwa na utambuzi wa magonjwa basi atakuwa na nafasi kubwa
ya kufanikiwa na kutimiza ndoto zake za maisha.
“Kundi hili kama lisipoangaliwa kwa makini na kupewa elimu
hii ya utambuzi juu ya mambo mbalimbali, ikiwemo elimu ya uzazi na kujikinga na
magonjwa linaweza kupoteza mwelekeo, ambao madhara yake huwa ni makubwa…lakini
pia athari zake husambaa kwa jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Mwalisu.
Aidha, kuhusu sera ya ulinzi na usalama wa mtoto, Mwalisu
alisema jamii inapaswa kutambua na kuheshimu takwa hilo la msingi la mtoto
kupata elimu, kuheshimiwa, kupendwa na kulindwa kama haki ya msingi na sio
hiari, lengo hasa ni kujenga ustawi na taswira chanya ya ukuaji wake
kisaikolojia na kiafya.
Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa
Singida, Yasinta Alute alisema afya njema ni matokeo ya kila kitu katika maisha
na ustawi wa ukuaji wa mtoto. Alisisitiza kama rika hilo la mtoto wa kile
likipatiwa mafunzo ya mara kwa mara juu ya utambuzi kwenye nyanja mbalimbali-
mfano wa hayo yanayowezeshwa na ‘Camfed’ ni dhahiri litageuka chachu katika kuleta
maendeleo kwenye jamii.
“Ukipata mafunzo ya afya ya uzazi na ukajitambua huwezi
kukosea wala kurudia tena makosa…nawaomba ninyi mliobahatika kupata mafunzo
hayo mkawe chachu na mabalozi kwa wengine,” alisema Alute huku akiwaomba Camfed
Makao Makuu kuangalia namna ya kupanua wigo wa huduma zao kwenye wilaya
nyingine mkoani hapa ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika.
Awali, Afisa Elimu Sekondari na Mwenyekiti wa Kamati ya
Wilaya ya Camfed Manispaa ya Singida, Omary Kisuda, alisema jumla ya wasichana
60 kutoka Singida Manispaa na wilaya ya Manyoni wanaendelea kupewa mafunzo
kupitia programu ya elimu ya utambuzi kwa mtoto wa kike yaani ‘Tanzania
Campaign for Female Education’
“Hili ni rika la wao kujiendeleza kielimu, biashara,
ujasiriamali, na elimu ya afya ya uzazi na ndio sababu hasa ya kuwakutanisha na
kuwapa mafunzo haya muhimu ya utambuzi chini ya ufadhili wa Camfed na
Serikali,” alisema Kisuda.