*************************************************
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa ili kuimarisha utawala bora na kuhakikisha haki ina tamalaki. Leo tunatoa taarifa za kuwafikisha wahalifu mahakamani; kurejesha fedha zilizookolewa; na uamuzi wa shauri lililokuwa Mahakamani.
Kwanza, Ijumaa tarehe 13/11/2020 tulimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Bw. Elibariki Yusto Mnghani (29) Mkazi wa Jijini Dodoma ambaye ni Afisa Uhamiaji na kumfungulia mashtaka mawili ya kushawishi na kupokea rushwa ya shilingi laki tano (500,000/=) kinyume na kifungu cha 15(1)a cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.
Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba majira ya saa 5 usiku wa tarehe 13/10/2020 katika eneo la Dodoma Hotel Jijini Dodoma, Mshtakiwa alishawishi na kupokea rushwa hiyo kutoka kwa Bw. Saurabh Tanwar kama kishawishi ili asaidie kuachiwa kwa Bw. Gangeswaran Thangadurai, raia wa India, ambaye alikuwa ameshikiliwa na Maafisa wenzake wa Uhamiaji kwa kosa la kuwazuia kufanya kazi yao.
Pili, tumemfikisha pia katika Mahakama hiyo Bw. Hamisi Hassani Athumani (27) Mkazi wa Jijini Dodoma ambaye ni Fundi magari wa kampuni ya Yapi Merkezi na kumfungulia mashtaka sita ya kushawishi na kupokea jumla ya shilingi laki tatu na elfu themanini (380,000/=) kutoka kwa wananchi watatu kinyume na kifungu cha 15(1)a cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007. Uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma umeonyesha kwamba kati ya Oktoba, 2019 na Januari, 2020, Mshtakiwa alipokea fedha hizo ili awasaidie wananchi hao kupata ajira katika kampuni anayofanyia kazi.
Tatu, tumemfikisha katika Mahakama ya Wilaya Kongwa Afisa Afya Mkuu Msaidizi wa Mamlaka ya Mji mdogo Kibaigwa Bw. Anania Joseph Madono (57) ambapo alifunguliwa mashtaka mawili ya kushawishi rushwa ya shilingi laki mbili (200,000/=) na kupokea shilingi laki moja na elfu sitini (160,000/=) kinyume na kifungu cha 15(1)a cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.
Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba mwanzoni mwa mwezi Novemba 2020, Mshtakiwa alikamata na kushikilia madumu 63 yenye lita 309 za mafuta ya alizeti mali ya Mtoa taarifa wetu kwa madai kwamba hayana taarifa za vifungashio (labels), na alimtaka ampe fedha ndipo ayaachie.
Tarehe 8/11/2020 alikamatwa eneo la Kibaigwa wilayani Kongwa baada ya kupokea rushwa na kumrejeshea Mtoa taarifa madumu yake ya mafuta aliyokuwa ameyashikilia ofisini kwake.
Nne, Vilevile TAKUKURU imerejesha jumla ya shilingi 21,276,800/= yakiwa ni madeni ya Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS); mkopo umiza; na mapunjo baada ya kuachishwa kazi. Kiasi cha shilingi 10,976,800/= kimerejeshwa na Ofisi yetu ya Kondoa kwa uongozi wa Mkombozi Soko Kuu SACCOS ya mjini Kondoa yakiwa ni madeni sugu ya wanachama 27 wa chama hicho yaliyokusanywa na TAKUKURU.
Kiasi cha shilingi 5,100,000/= kimerejeshwa kwa Askari Magereza Mstaafu Bw. Julius Francis Mtono baada ya TAKUKURU kuitaka kampuni ya Kihega Investment LTD inayofanya biashara ya kukopesha fedha Jijini Dodoma kurejesha fedha hizo ilizojipatia kinyume na makubaliano baada ya kumpatia Bw. Mtono mkopo wa shilingi 6,000,000/= Septemba, 2017. Baada ya mafao ya kustaafu ya Bw. Mtono kutoka Oktoba, 2018, uchunguzi umebaini kwamba kampuni hiyo ilikata fedha nyingi zaidi na ufuatiliaji wa TAKUKURU umewezesha kurejeshwa kwake.
Pia tumewezesha Bi. Rehema Ramadhani Shembuli kulipwa na aliyekuwa Mwajiri wake kampuni ya Traveling-Link tawi la Dodoma, mafao yake ya shilingi 5,200,000/= aliyostahili baada kuachishwa kazi. Awali kampuni hiyo haikumlipa chochote hadi alipotoa taarifa kwetu ambapo baada ya kufuatilia ndipo kiasi tajwa kikalipwa.
Tano, Mahakama ya wilaya ya Bahi imetoa uamuzi wa shauri la jinai namba 46/2019 na kumhukumu Bw. Daudi Masigati, Mjumbe wa Baraza la Ardhi Kata ya Chikola-Bahi aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya kushawishi na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)a cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa namba 11/2007, kulipa faini ya shilingi laki tano (500,000/=) au kwenda jela kwa miaka mitatu kwa kila shtaka. Uamuzi huo umetolewa baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na TAKUKURU kufuatilia uchunguzi ulionyesha kwamba mwaka jana alishawishi na kupokea shilingi 200,000/= ili amsaidie mtoa taarifa wetu kushinda shauri lake la mgogoro wa ardhi lililokuwa linaendelea kwenye Baraza.
Mwisho tunapenda kuwaasa wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuwa makini na matapeli wanaojifanya Maafisa wa TAKUKURU na kamwe kutokubali kuitikia wito wa kuwasilisha nyaraka au kukutana nje ya ofisi yetu ya Mkoa na zile za Wilaya. Huduma za TAKUKURU ni bure hivyo kamwe msidanganywe kulipa chochote. Tunawaomba mtoe taarifa Ofisini pale mnapokutana na hali yoyote ya kuwatia shaka.