Wahamiaji wasiopungua 74 wamekufa katika ajali mbaya ya meli iliyotokea katika pwani ya Libya. Shirika la IOM limesema manusura 47 wameweza kuokolewa wakati shughuli ya uokozi zikiendelea.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, wahamiaji wapatao 74 wamefariki dunia baada ya meli kuzama hapo jana nje ya pwani ya Libya.
Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema boti hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya watu 120, kati yao wanawake na watoto.
Aidha limeongeza kuwa manusura 47 wameweza kuokolewa na miili 31 tayari imeopolewa.
Shirika la IOM limeeleza kuwa tangu mwezi Oktoba, hii ni takriban ajali ya tisa kutokea katika bahari ya Mediterania. Na katika siku mbili zilizopita, watu wasiopungua 19, pamoja na watoto wawili, walizama baada ya boti mbili kuzama katikati mwa bahari ya Mediterania.
Zaidi ya wahamiaji 20,000 wamekufa katika miaka saba iliyopita, kulingana na shirika hilo la uhamiaji la Umoja wa Mataifa.
Wafanyabiashara haramu ya kusafirisha binadamu wamezitumia vurugu hizo zinazoendelea nchini Libya, kuigeuza nchi hiyo kuwa njia kuu kwa wahamiaji wanaokimbia vita na umaskini wakiwa na tamaa na kufika Ulaya.
Machafuko yalizuka nchini humo mnamo mwaka 2011, wakati alipoondolewa madarakani na kuuliwa kiongozi wa muda mrefu Moamer Kadhafi.
Wahamiaji wengine wakamatwa na kurudishwa Libya
Maelfu ya wahamiaji wengine hukamatwa na walinzi wa pwani ya Libya, ambao wanaungwa mkono na Italia na Umoja wa Ulaya. Baada ya kukamatwa wahamiaji hao hurudishwa Libya na kuwekwa katika vizuizi vyevye hali mbaya.
Wahamiaji katika bahari ya Mediterania
Makundi ya kuteeta haki za binadamu yameikosoa sera hiyo, na shirika la IOM limefanya kampeni ya kutaka kukomesha utaratibu wa kuwarudisha wahamiaji hao Libya, iliyo kilomita 300 kutoka pwani ya Italia.
Ajali hiyo ya kuzama meli imetokea wakati wajumbe wa Libya wakiwa wanashiriki mazungumzo ya kisiasa nchini Tunisia yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza mapigano ya miaka kadhaa ya Libya, kuundwa serikali ya mpito na kuandaliwa uchaguzi wa rais na bunge utakaokuwa huru, wa haki, utakaozijumuisha pande zote na utakaokuwa wa kuaminika.
Tangu kuondolewa na kuuawa kwa Kadhafi, Libya yenye utajiri wa mafuta imekumbwa na machafuko na ghasia, huku serikali hasimu za mashariki na magharibi zikigombania udhibiti wa nchi hiyo.
Mazungumzo ya kisiasa nchini Tunisia yanafanyika kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa mnamo mwezi Oktoba.
Wakati huo huo kunafanyika mazungumzo ya kijeshi katika mji wa Libya wa Sirte, ambayo pia yanaongozwa na Umoja wa Mataifa.