Watendaji wa Mfuko wa Taifa wa Maji wakikagua ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye lita za ujazo 1000 katika mradi wa Kirando uliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Tanki la kuhifadhia maji lenye lita za ujazo 1000 lililojengwa na wataalam wa ndani katika mradi wa maji wa Kirando uliopo Nkasi mkoani Rukwa.
……………………………………………………………………………
Wananchi zaidi ya elfu 70 wa vijiji vya Kirando na Katete katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wataanza kupata huduma ya majisafi na salama baada ya siku 60 kuanzia sasa ambapo mradi wa maji wa Kirando ambao umefikia asilimia 85 ya ujenzi kukamilishwa.
Mradi wa maji wa Kirando unatekelezwa na Serikali kwa kutumia wataalam wa Wizara ya Maji kwa utaratibu wa force account kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) na hadi sasa ujenzi wake umetumia kiasi cha shilingi bilioni 1.5
Mhandisi Anna Kavuruga wa SUWASA akiongea na watendaji wa Mfuko wa Maji amesema kazi ya utekeleaji wa mradi imehusisha pamoja na mengine, ujenzi wa chanzo, ujenzi wa jengo la pampu na kufunga pampu, na ujenzi wa vituo vya kutoa huduma ya majisafi kwa wananchi vipatavyo 50 na thamani ya mradi ni kiasi cha shilingi bilioni 3.5.
Mradi wa maji wa Kirando utakaotumia maji ya Ziwa Tanganyika ulianza kutekelezwa tarehe 1 Septemba 2019, kwa fedha iliyotolewa na Mfuko wa Maji wa Taifa umetekelezwa kwa wakati na wananchi watapata huduma ya maji kama ilivyopangwa na Serikali.
Pamoja na mradi wa maji wa Kirando, Mfuko wa Maji wa Taifa umetoa fedha za utekelezaji wa mradi wa maji wa Namanyere ambao utaboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 20 hadi kufika asilimia 80 katika mji wa Namanyere. Mradi wa Maji wa Namanyere umefika asilimia 60 ya utekelezaji na kukamilika kwake kutanufaisha zaidi ya wakazi elfu 18.