Na.Alex Sonna,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli amesema kipindi cha miaka mitano ijayo serikali yake imepanga kuendeleza miundo mbinu kwa kununua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya bustani, minofu ya samaki na nyama lengo ni kuwafanya wakulima watajirike kutokana na kazi wanayofanya.
Rais Dk Magufuli ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 12 huku akilihutubia bunge hilo na Taifa kwa ujumla na kusema kuwa lengo lake ni kuona kila mtanzania ananufaika na maendeleo ya ukuaji uchumi nchini.
Aidha Rais Magufuli amesema kuwa serikali yake imepanga kuongeza tija kwenye kilimo kwa kukifanya kuwa cha kibiashara lengo likiwa kuwa na hifadhi kubwa ya chakula, malighafi za viwandani na kuuza pia nje ya nchi hivyo upatikanaji wa mbegu na zana za kilimo zitaboreshwa.