Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, (pili kulia) akitoa maelekezo kwa ujumbe aliombatana nayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ua usambazaji wa umeme vijijini katika moja ya vijiji wilayani Mbinga mkoani Ruvuma,Novemba 10-11,2020.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (mwenye miwani),akipitia taarifa ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, 10-11,2020.
Msimamizi wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini kutoka kampuni ya NAMIS, mhandisi Joseph Lipuka( kushoto) akimuonyesha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja( pili kushoto) pamoja na ujumbe alioambatana nao kutoka REA na TANESCO, njia itakayopitiwa na miundombindo ya umeme katika Wilaya ya Namtumbo( haionekani pichani) wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu huyo ya kukagua Maendeleo ya Usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya za Mkoa wa Ruvuma, Novemba 10-11,2020.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja,(pili kulia) akitoa maagizo kwa ujumbe aliombatana nayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,Novemba 10-11,2020.
**************************************
Zuena Msuya – Ruvuma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja amewaagiza watendaji wa kampuni ya ukandarasi ya Namis Corporate Ltd, wanaotekeleza mradi wa umeme vijijini (REA), mkoani Ruvuma, kuongeza kasi ili wakamilishe kazi hiyo kwa wakati.
Alitoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mkoani Ruvuma, Novemba 10 hadi 11 mwaka huu.
Mhandisi Masanja alimtaka mkandarasi huyo kufanya kazi kwa ubunifu na viwango huku akiiga mifano ya kampuni nyingine za ukandarasi ambazo zinafanya kazi nzuri.
Akifafanua kuhusu ubunifu, Naibu Katibu Mkuu alimwelekeza mkandarasi huyo ambaye utendaji kazi wake unasuasua, kunu nua vifaa hivyo hapa nchini kwa vinapatika, kuazima kutoka kampuni nyingine za ukandarasi au Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) badala ya kutumia muda mrefu akisubiri vifaa alivyoagiza nje ya nchi.
“Azimeni vifaa mnavyovihitaji kutoka kwa wenzenu ili muendelee na kazi na mtawarudishia vifaa hivyo pindi mlivyoagiza vitakapofika. Nasisitiza kuwa hakuna sababu ya msingi inayosababisha mradi kutotekelezwa kwa wakati,” alisisitiza.
Aidha, alimtaka mkandarasi husika kuongeza nguvu kazi pamoja na kulipa stahili za wafanyakazi na vibarua kwa wakati hali ambayo alisema itaongeza morari yao ya utendaji kazi na hivyo kuwezesha kazi kukamilika kwa wakati na viwango stahiki.
Mhandisi Masanja alimuagiza msimamizi wa Mradi wa Mkandarasi kuhakikisha anakuwepo katika eneo la mradi wakati wote kwa ajili ya kusimamia na kukamilisha kazi za mradi kwa wakati.
Vilevile TANESCO na REA kuhakikisha wanatembelea maeneo ya mradi kuanzia tarehe 16 Novemba, 2020 ili kujiridhisha kama Mkandarasi ametekeleza maagizo ya Serikali ya kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kasi inayotakiwa.
REA iangalie uwezekano wa kujumuisha kwenye mradi vifaa vyote vinavyohitajika katika ufungaji wa Umeme Tayari( UMETA) ili kuwezesha kuwaunganishia umeme wateja wengi hususan wenye kipato kidogo.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu aliambatana na Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Christopher Bitesigirwe, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu pamoja na viongozi kadhaa wa TANESCO mkoani Ruvuma.