**********************************************
⦁ Hafla hiyo ina lengo la kuchangisha fedha ambazo zitaelekezwa kusaidia utengenezaji wa maktaba ya watoto na kununua vifaa vya matibabu ya watoto njiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH).
Taarifa iliyotolewa leo Novemba 12, 2020 kwa vyombo vya habari inaeleza kwamba Mpango wa Beauty Legacy Tanzania unaowaleta pamoja washika taji la Miss Tanzania kuhamasisha wadau mbalimbali kusaidia sekta za afya na elimu imetangaza tarehe ya hafla ya kuchangisha misaada itakayofanyika Desemba 12, 2020.
Akizungumza leo Novemba 12,2020 jijini Dar es Salaam, Mjasiriamali na Mwanzilishi wa Dkt.Ntuyabaliwe Foundation, Bi Jaqueline Mengi alisema amevutiwa kuwaleta pamoja washindi wa zamani na washiriki wa shindano la urembo la Miss Tanzania ili kukusanya fedha wa kusaidia jamii.
Alisema kuwa hafla hiyo ambayo awali ilikuwa imepangwa kufanyika Novemba 14,2020 , sasa itafanyika Desemba 12,2020.
Jacqueline ambaye pia ni Mdhamini wa Taasisi ya Dk.Reginald Mengi People with disabilities Foundation alisema,”Tunafurahi sana kuwa Rais Mstaafu Dkt. Kikwete amekubali kuwa Mgeni wa heshima katika hafla ya kukusanya fedha za BEAUTY LEGACY GALA 2020.
“Tunamshukuru sana kwa kutuunga mkono katika hafla yetu iliyopangwa kufanyika Desemba 12 mwaka huu. Tunawashukuru pia wachangiaji wote ambao wanaunga mkono azma hii,”alisema Jacqueline.
Alisisitiza fedha zitakazopatikana zitaelekeza kusaidia kutengeneza maktaba ya watoto pamoja na kununua vifaa vya kusaidia maisha kwa watoto waliozaliwa mapema (njiti) katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Jacqueline alisema katika hafla hiyo zaidi ya wadau 200 wakiwemo wafanyabishara wenye ushawishi , benki, wasanii , viongozi wa jamii, maofisa wa serikali, wafadhili wa ushirika, NGOs, mabalozi,madaktari, na wafadhili mbalimbali watashiriki tukio hilo kubwa la kihistoria litakalofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Kauli mbiu katika tukio hilo inaeleza hivi ” KUJENGA MATUMAINI, KUJENGA MAISHA, KUJENGA BAADAE.”
KUHUSU BEAUTY LEGACY GALA
Akifafanua kuhusu Beauty Legacy Gala 2020, ni hafla ya hisani ya kukusanya fedha na ni usiku wa shamrashamra za aina yake ikiongozwa na yeye Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi pamoja na washindi wa zamani wa shindano la Miss Tanzania.
“Tukio hilo limehamasishwa na maisha ya nyakati za historia ya miaka 20 tangu Jacqueline Ntuyabaliwe apate taji la Miss Tanzania mwaka 2000, unakosaje kosaje?Hii ndio nafasi yako ya kuwa sehemu ya Tanzania Beauty Legacy Gala 2020 kutafuta misaada ya hisani ambayo itakusanya fedha kwa ajili ya watoto na wanawake wenye uhitaji maalum,”alisema.
Alifafanua siku hiyo itakuwa fursa adhimu ya kusikia hadithi za kutia moyo kutoka kwa malkia hao wa urembo na wafadhili wanaoambatana nao.Hata hivyo Malkia wa zamani wa taji la urembo wataonesha talanta zao.