Waziri Mkuu Mteuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa akiwashukuru wabunge waliomchagua kwa kishindo wakati wa Bunge la 12 Jijini Dodoma
………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri Mkuu Mteule Kassim Majaliwa ametoa shukrani zake kwa Rais Dk John Magufuli kwa kumuamini na kumpendekeza kushika nafasi hiyo ikiwa ni muda mchache mara baada ya jina lake kupitishwa na wabunge wote kwa asilimia 100
Mapema leo leo jijini Dodoma Mpambe wa Rais Magufuli alileta jina la Kassim Majaliwa akimpendekeza kuwa Waziri Mkuu ambapo wabunge walipiga kura ya kulithibitisha jina hilo na kati ya kura 350 zilizopigwa na wabunge zote zilimpigia kura za ndio kwa asilimia 100.
Akizungumza baada ya kupitishwa na Bunge, Majaliwa amewatoa hofu wabunge na kusisitiza kuendeleza mshikamano ili kutimiza ndoto ya serikali ya awamu ya tano
Amesema imani hiyo aliyooneshwa na Rais Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na namna bunge lilivyomuidhinisha basi ana wajibu mkubwa wa kuitunza na kuilinda imani hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu sambamba na kutanguliza uzalendo mbele katika kuwatumikia watanzania na kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho kinachounda serikali.
” Jambo hili la kunipitisha kuwa Waziri Mkuu siyo dogo ninaamini Mwenyezi Mungu ameliongoza, nimshukuru Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyonayo juu yangu kuendelea kuniamini kwa Kazi kubwa tuliyofanya pamoja.
Nafahamu Rais kwa mamlaka yake anaweza kumshirikisha Makamu wa Rais katika maamuzi kama haya, nimshukuru pia Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia jina langu katika nafasi hii na kuniamini tena, sina hakika kama neno hili la shukrani linatosha lakini mimi na familia yangu na wananchi wangu wa Ruangwa tunashukuru sana,” Amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema anamhakikishia Rais Magufuli kwamba ataendelea kufanya kazi kwa spidi ile ile na atailinda imani aliyomuonesha huku akimsaidia kazi kadri Mwenyezi Mungu atakavyomuongoza.
” Nikushukuru sana wewe Spika na Bunge lako kwa kunipigia kwa kura nyingi za ndio haijawahi kutokea, nitaendelea kushirikiana nanyi, kupokea changamoto zenu, kuzitatua na tutakuja huko majimboni kwenu kushirikiana nanyi katika kuwatumikia watanzania ambao wametuamini na kutuchagua,” Amesema Majaliwa.