Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa wakiwa kwenye banda wakisubiri kuingia mahakamani kusikiliza maombi yao ya marejeo ya kesi dhidi ya Bodi ya Thaqaafa, kushoto na Katibu wa Bodi hiyo Alhaji Abdallah Amin na kushoto ni mmoja wa wadau wa msikiti huo Nurdin Anasa.Mjumbe wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa, Hussein Sherally (kushoto)katikati ni Nurdin Anas mmoja wa dawau na nyuma kutoka kushoto ni katibu wa Bodi hiyo Alhaji Abdallah Amin na na kwanza kushoto ni Daud Mkama.Picha zote na Baltazar Mashaka.
**********************************
MAHAKAMA Kuu ya Mwanza imeahirisha shauri la maombi ya Marejeo (Riview) namba 2 ya 2020 yaliyofunguliwa na Bodi ya Msikiti wa Ijumaa dhidi ya Bodi ya Wadhamini waandikishwa wa Shule ya Thaqaafa.
Maombi hayo yalifunguliwa mwaka huu na Bodi ya Msikiti wa Ijumaa kuhusu uamuzi wa mahakama hiyo uliotokana na rufaa namba 10/2020 na uliyoipa ushindi Bodi ya Wadhamini wa Thaqaafa.
Maombi hayo yanayosikilizwa na Jaji A.Z. Mgeyekwa wa Mahakama Kuu Mwanza,yaliahirishwa jana hadi Novemba 25, mwaka huu baada ya wakili wa wajibu maombi kuomba muda ili kupitia vielelezo vya waleta maombi na kuyajibu.
Kabla ya kuahirishwa kusikilizwa kwa maombi hayo, Wakili wa wajibu maombi Wilbert Kilenzi, aliiomba mahakama akisema maombi hayo yameambatanishwa na kiapo chenye mambo makubwa ya kisheria hivyo wapewe muda kuweza kuyapitia na kuyajibu.
“Mheshimiwa Jaji,maombi haya ya marejeo yana vitu vingi ambavyo tuna wajibu wa kuvi account ili kuweza kuisaidia mahakama yako, pia kesi hii ina mapungufu ya kisheria hivyo tunaomba upange tarehe nyingine tupate muda wa kuvipitia,”aliomba Kilenzi.
Wakili wa waleta maombi Godfrey Samson wa LZone Allied Advocate anayesaidiana na Steven Henga, alisema hawana pingamizi na kuomba pia wapewe muda wa ku amend (kusahihisha au kuboresha baadhi ya vitu).
“Shauri hili lilikuja kwa kusikilizwa na hatuna pingamizi na prayer (ombi) ya mjibu maombi,tunaomba muda wa kurekebisha na kuongeza baadhi ya vitu kwenye maombi ya wateja wetu, ”alisema Godfrey.
Jaji Mgeyekwa alikubaliana na hoja za mawakili wa pande zote na kuahirisha shauri hilo hadi Novemba 25, mwaka huu siku ambayo maombi yao yatasikilizwa ambapo kabla kila upande utatakiwa kupeana nakala za majibu yao Novemba 17, mwaka huu.
Awali Bodi ya Thaqaafa ilifungua kesi namba 11/2019 kwenye Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana ikipinga kulipa kodi ya pango sh. milioni 58 baada ya kuingia mkataba wa upangaji na Bodi ya Msikiti wa Ijumaa Machi, 2015 kwamba licha ya kuwa ni wapangaji haikustahili kulipa.
Hakimu Gwaye Sumaye akitoa hukumu ya shauri hilo aliitaka bodi hiyo kuheshimu mkataba wa upangaji wa 2015 ambapo baada ya kushinda kesi Bodi ya Msikiti wa Ijumaa ilikaza hukumu na kupata Decree (agizo/amri).