KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao.
************************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimepongeza hotuba iliyotolewawa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,kuwa imetafsiri muelekeo halisi wa maendeleo endelevu ya nchi chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nane ya Zanzibar.
Hotuba hiyo ilitolewa jana (juzi) na Rais Dk.Hussein, wakati akizindua Baraza la kumi mkutano wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar huko katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.
Kimeeleza kwamba hotuba hili licha ya kufafanua kwa kina namna serikali itakavyopaisha uchumi wa nchi, bali pia imezingatia maslahi ya makundi yote ya kijamii.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar Catherine Peter Nao, wakati akizungumza katika mahojiano maalum huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Alisema kupitia hotuba hiyo Rais Dk.Hussein,alieleza kwa kina namna watakavyonufaika wananchi na rasilimali za taifa huku akiahidi kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,kijamii na kisiasa.
Katibu huyo wa Idara ya itikadi na Uenezi Catherine, alieleza kuwa Rais ameahidi kuijenga Zanzibar mpya kupitia uchumi wa kisasa wa buluu (blue Economy) unaopatikana kupitia rasilimali ya bahari.
Katibu huyo alisema kupitia uchumi huo wa bahari unaofungamanisha sekta mbalimbali zikiwemo uvuvi,ufugaji wa kisasa wa samaki,ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki,ukulima wa mazao ya baharini ikiwemo mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi pamoja na sekta ya utalii zote hizo zitatoa ajira za kudumu kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Katika maelezo yake Catherine, alisema yote yaliyoelezwa na Rais Dk.Hussein, yameelekezwa kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa lengo la kuhakikisha yanafanyika mapinduzi ya kiuchumi yatakayoifikisha Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi chache za visiwa zenye uchumi mkubwa Duniani.
“CCM Zanzibar inampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hotuba yake iliyoonyesha dhamira,dira,mipango endelevu na malengo halisi ya Serikali ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar bila ubaguzi wa rangi,kabila na itikadi za kisiasa kwani maendeleo hayana Chama.”, alisema Catherine.
Alisema CCM imekuwa ni Chama cha kisiasa cha kwanza nchini Tanzania toka kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992, kilichoeleza kupitia miongozo ya Kikanuni, Kikatiba na machapisho yake mbalimbali kuwa kinachukia vitendo vya rushwa na ufisadi jambo ambalo Rais Dk.Hussein ameahidi kudhibiti vitendo hivyo vinavyokwamisha maendeleo.
Pamoja na hayo alisema Rais alionyesha nia ya dhati katika utawala wake kufuata misingi ya haki za binadamu na utawala bora mambo ambayo ndio yamekuwa ni kielelezo cha mafanikio yaliypatikana baada ya kufanyika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“Misingi ya utawala bora iliasisiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi marehemu Abeid Amani Karume, aliyeondosha vitendo vya uonevu kwa wazawa na kuasisi utamaduni wa haki,utu na ustawi wa kijamii”, alifafanua Katibu huyo.
Aidha Catherine alimpongeza Rais Dk.Hussein, kwa kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali watakaomsaidia katika safari yake ya kuijenga nchi kiuchumi na kwamba uteuzi huo hauna shaka kwani umezingatia vigezo na sifa za walioteuliwa kwa mujibu wa majukumu waliopangiwa.
Alisema CCM inawataka viongozi na watendaji mbalimbali waliopewa dhama za uongozi kutekeleza wajibu kwa kasi na matarajio ya Rais Dk.Hussein ili wananchi waliowachagua kwa kura nyingi waendelee kukiamini Chama.
Akizungumzia matarajio ya CCM kwa serikali mpya ya awamu ya nane Catherine, alisema kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mhe.Hemed Suleiman Abdalla wataivusha na kuipandisha hadhi nchi kwani ni viongozi vijana,wasomi,wathubutu,wanajiamini na wenye misimamo isiyoyumba,makada waliofunzwa uzalendo na wana uzoefu mkubwa katika masuala ya uongozi.
Pamoja na hayo Katibu huyo, alisema kwamba Rais Dk.Hussein ni miongoni mwa viongozi wanaotambua na kuheshimu tunu za taifa ambazo ni Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano pamoja na Uhuru tunu zilizoasisiwa na waasisi wa Taifa ambao ni Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Aman Karume.
Rais Dk.Hussein, huo ni mkutano wake wa kwanza kuhutubia wa wa Baraza hilo toka alipochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kupitia ushindi wa kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 katika uchaguzi mkuu wa dola wa Octoba 28, mwaka 2020 uliofanyika kwa uwazi,uhuru na Demokrasia kubwa visiwani Zanzibar.