Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.
…………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imemtaka mkurugenzi wa kampuni ya Namaingo Business Agency ya jijini Dar es salaam, Biubwa Ibrahim kuwarudishia wajasiriamali 300 wa Wilayani Hanang’ shilingi milioni 42 walizozichukua mwaka 2017.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu ameyasema hayo Novemba 9 Mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Makungu amesema TAKUKURU Mkoani Manyara imeanza kuchukua hatua baada ya Rais John Magufuli kuagiza vitendo vya dhuluma na rushwa kukomeshwa.
“Octoba 25 akiwa kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati, Rais John Magufuli alitoa ahadi mbalimbali ikiwemo kutokomea vitendo vya dhuluma na rushwa,” amesema Makungu.
Amesema TAKUKURU inafanya uchunguzi juu ya kampuni ya Namaingo na mkurugenzi huyo Biubwa na baadhi ya maofisa wa serikali wasiokuwa waaminifu walichukua fedha za wajasiriamali hao tangu mwaka 2016 wakidai kuwafanyia semina.
Amesema katika semina hiyo wajasiriamali hao walitakiwa kujiunga katika vikundi vya watu 50 na kila mwana kikundi alitakiwa kuandaa banda la kuweka vifaranga vya kuku 1,000 na kuahidi kuwapatia vifaranga 1,000 kama mtaji.
Amesema viongozi wa kampuni hiyo waliwaahidi wajasiriamali hao kuwapatia chakula, dawa za kuwakinga na ugonjwa vifaranga hao hadi kufikia hatua ya kufikishwa sokoni na watawatafutia masoko.
“Baada ya maelezo hayo ya kuvutia kutoka kwa viongozi wa Namaingo wajasiriamali hao kila mmoja alitakiwa kulipa shilingi 140,000 kwa mchanganuo mbalimbali,” amesema Makungu.
Amesema Kati ya fedha hizo shilingi elfu 50 ni ya kiingilio, shilingi elfu 46 ya usajili wa BRELA, shilingi elfu 20 kwa ajili ya ukaguzi wa maeneo ya kufugia vifaranga, shilingi elfu 20 za gharama ya kuingia mkataba na shilingi elfu 5 ya kufungulia faili.
Amesema viongozi wa Namaingo baada ya kupokea fedha hizo walitoweka na wajasiriamali hao walipofuatilia fedha zao hawakufanikiwa na kubaini wamefanyiwa udanganyifu.
“Takukuru Mkoani Manyara tunamtaka mkurugenzi wa kampuni ya Namaingo Biubwa popote alipo ajisalimishe na kurudisha fedha za wajasiriamali hao kabla ya Novemba 30 kwani baada ya hapo watawachukulia hatua,” amesema Makungu.
Amewataka wajasiriamali hao waliochukuliwa fedha zao wafike na nyaraka zinazoonyesha kwenye ofisi za TAKUKURU Wilayani Hanang’ na aliyembali atume nyaraka kwa barua pepe [email protected] ili madai yao yaweze kufanyiwa kazi kwa pamoja.