Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Nsemulwa katika Manispaa ya Mpanda akiwa ofisini kwakeBaadhi ya wanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Nsemulwa wakielekea darasani baada ya muda wa mapumziko kuisha.
****************************************
Na Zillipa Joseph, Katavi
Jumla ya wanafunzi 3370 wa shule ya msingi Nsemulwa iliyopo katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wameondokana na adha kufuatilia masomo wakiwa nje ya vyumba vya madarasa kutokana na uchache wa vyumba hivyo
Mapema mwaka uliopita mwandishi wa habari hizi alifika shuleni hapo na kukuta baadhi ya wanafunzi wakiwa wamesimama madirishani wakifuatilia masomo kutokana na darasa kujaa wanafunzi kiasi cha kuufikia ubao
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Emmanuel Said Mbogo amesema hali hiyo ilipelekea wanafunzi wa darasa la tatu, nne na tano kusoma nyakati za mchana huku madarasa mengine wakisoma asubuhi
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamejenga vyumba saba vya madarasa na hivyo kufanya shule hiyo kuwa na jumla ya vyumba kumi na nane vya madarasa kutoka vyumba kumi na moja vilivyokuwepo awali
“Sasa hivi hata walimu wanapata nafasi nzuri ya kupumzika tofauti na awli ambapo walilazimika kuingia kwa zamu, ufundishaji wa mchana ni mgumu kwani baadhi ya wanafunzi wanakuja shule bila ya kupata chakula kwa hiyo kuelewa inakuwa changamoto” alisema mwalimu Mbogo
Aidha ameongeza kuwa wamepata shilingi milioni arobaini ambazo watajenga madarasa matatu katika shule shikizi ya mtaa wa Tulieni ili kuendelea kupunguza msongamano madarasani
“Shule hii imechukua mitaa sita, kwa kujenga shule shikizi Tulieni itasaidia wanafunzi wa upande ule kusomea kulekule waliko” alisema