**********************************
Na John Walter-Manyara
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara imeanza kufanyia kazi ahadi iliyotolewa na Rais Dr. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha Rushwa na dhuluma za aina zote zinatokomezwa.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu amewaambia waandishi wa Habari kuwa wameanza kutekeleza ahadi hiyo kwa kufanyia kazi taarifa walizopokea kutoka kwa baadhi ya wakulima wilaya ya Hanang’.
Makungu ameeleza kuwa mnamo mwaka 2016 kampuni iitwayo Farm Green Implements T. Ltd inayomilikiwa na Dunga Othman Omar, ilikusanya fedha kutoka kwa baadhi ya wakulima kwa ahadi za kuwaletea Matrekta ahadi ambayo haikutekelezwa hadi sasa.
Mkuu huyo wa Takukuru ameeleza kuwa wamepokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi wawili ambapo mmoja wao alitoa kiasi cha shilingi Milioni Kumi na saba (17,000,000) na mwingine alitoa Shilingi Milioni Kumi na Sita na Laki Mbili (16,200,000).
Uchunguzi wa Takukuru mkoani Manyara umebaini kuwa fedha hizo zote Dunga alizielekeza kwenye akaunti yake binafsi badala ya kampuni jambo ambalo linaashiria nia ovu katika kujipatia fedha hizo ambapo kwa sheria zilizopo anaweza kushtakiwa kwa makosa ya jinai yakiwemo ya kujipatia fedha kwa udanganyifu kisha kutakatisha fedha hizo.
“Ninamtaka Dunga Othman Omar popote alipo aziwasilishe fedha hizo kwa mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara kabla ya tarehe 18 Novemba 2020 ili ziweze kufanyiwa utaratibu wa kurejeshwa kwa wakulima hao” alisisitiza Makungu
Kwa upande mwingine amewataka wananchi wengine ambao fedha zao zilichukuliwa na Dunga Othman kwa udanganyifu wa kuletewa Trekta na hawakuletewa wawasilishe malalamiko yao kupitia namba ya dharura 113 au namba ya mkononi ya Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara 0738150124 ili yafanyiwe kazi kwa pamoja.