*************************************
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inapenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuapishwa Novemba 5, 2020 ili kuendelea kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Kuchaguliwa kwa Mhe. Magufuli kwa mara ya pili kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni ishara ya matumaini mema na imani ya hali ya juu waliyonayo wananchi wa Tanzania kwake.
Aidha, ni utambuzi siyo tu wa uwezo alionao, bali pia kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015 – 2020) ambapo Taifa letu limeshuhudia ongezeko la maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaendelea kuwa na matumaini makubwa na uongozi wake katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii, sambamba na kulinda, kuhifadhi na kutetea haki za binadamu, utawala bora, utawala wa sheria na uwajibikaji.
Tume inatambua kuwa dhamana aliyopewa Mhe. Rais na Watanzania ni kubwa. Ili kuitekeleza kikamilifu dhamana hii inahitaji kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu na ushirikiano wa Watanzania wote. Tume inamwomba Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, hekima na maarifa zaidi ya kuweza kulitumikia Taifa letu.
Tume inaamini kwamba baada ya Mhe. Rais kuapishwa mchakato wa uchaguzi umekwisha. Kilichobaki mbele yetu hivi sasa ni mshikamano na ushirikiano katika kuijenga nchi yetu. Hivyo, Tume inatoa wito kwa Watanzania na wadau wote wa maendeleo kutoa ushirikiano na kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mwisho, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inawatakia kila la kheri Mhe. Rais Magufuli pamoja na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu yao katika kipindi cha miaka mitano kilicho mbele yetu, 2020 – 2025.