Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara (MAMEC) Zacharia Mtigandi (kushoto) akimkabidhi mpira wa miguu mwanachama wa klabu hiyo Peter Ringi baada ya kununua mipira miwili kwenye ofisi za chama hicho Mjini Babati.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara (MAMEC) Zacharia Mtigandi (kushoto) akimkabidhi mpira wa pete mwanachama wa klabu hiyo Mariam Juma.
***********************************
WAANDISHI wa habari wa Mkoa wa Manyara, wametakiwa kujihusisha na michezo ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kuliko kuandika habari za michezo bila kushiriki.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara (Mamec) Zacharia Mtigandi ameyasema hayo wakati akigawa mipira kwa waandishi wa habari wa klabu hiyo.
Mtigandi amesema Mamec imenunua mipira miwili hivyo waandishi wa habari waitumie na siyo kubakia kuandika habari za michezo za watu wengine.
Amesema mipira hiyo miwili iliyonunuliwa ni mpira wa miguu, mpira wa pete na pampu ya kujaza upepo.
“Mipira hii itaazimishwa bure kwa mwanachama anayetaka kuitumia kwa mazoezi yake au na wenzake ili kuweka mwili kwenye hali mzuri kuliko kukaa hivi hivi kisha wanairudisha ofisini” amesema Mtigandi.
Hata hivyo, amewataka wanachama hao kutunza vifaa hivyo ipasavyo na kurejesha wakishavitumia na endapo mwanachama akiharibu anawajibika kutengeneza.
Katibu wa Mamec, Jaliwason Jason amewataka wanachama hao kutumia mipira hiyo ili kuunganisha umoja na upendo kwani michezo ni furaha.
“Pamoja na hayo michezo pia ni afya kwani ukikimbia kwenye mazoezi au mashindano utatoka jasho na kuondokana na magonjwa ya moyo kisukari na shinikizo la damu,” amesema.
Mmoja kati ya waandishi wa habari mwanachama wa Mamec, Peter Ringi amesema watatumia mpira huo kwa kucheza soka kwa lengo la kujiburudisha na kufanya mazoezi.
Mwanachama mwingine wa Mamec, Mariam Juma amewashukuru viongozi kwa kununua mpira wao kwani waandishi wasichana na wanawake watacheza mpira wa pete.