Rais mpya wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Erick Kisanga akizungunza na waandishi wa habari jijini Arusha muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuapishwa rasmi kuongoza tena kipindi cha miaka mitano katika sherehe iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu wa Umoja huo, Stellah Joel.
Katibu wa Umoja huo, Stellah Joel (kushot), akizungumza katika mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale
UMOJA WA Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) umempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mingine mitano kuanzia leo baada ya kuapishwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais mpya wa umoja huo Erick Kisanga wakati akizungunza na waandishi wa habari jijini Arusha muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuapishwa rasmi katika sherehe iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Rais Magufuli amekwisha apishwa kwa ajili ya kuwaongoza watanzania kwa kipindi kingine cha pili sisi wanamuziki tunakila sababu ya kumpongeza” alisema Kisanga.
Kisanga alisema kuchaguliwa kwake kwa kishindo kunatoka na imani ya wananchi waliyokuwa nayo katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano ambayo amefanya mambo makubwa ya mandeleo hapa nchini katika maeneo mbalimbali.
Kisanga alitaja baadhi ya mambo aliyoyafanya kuwa ni umeme, miundombinu ya barabara, shule, ujenzi wa reli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa vivuko, ujenzi wa zahanati na hospitali pamoja na miradi mingine mingi.
“Kutokana na kazi hiyo kubwa aliyoifanya wananchi wakiwepo wanamuziki walikuwa na kila sababu ya kumchagua kwa kura nyingi” alisema Kisanga.
Kisanga alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya usalama kwa kusimamia uchaguzi huo ambao ulifanyika kwa amani na utulivu.
Katibu wa Umoja huo, Stellah Joel aliwaomba wanamuziki kuendelea kutunga na kuimba nyimbo za kuhamasisha maendelea ya nchi ikiwa ni kuunga mkono jitihada za maendeleo za Rais Dkt.John Magufuli kuanzia awamu yake ya kwanza na hii ya pili ambayo ameianza leo.
Joel aliwataka wanamuziki kote nchini kubuni miradi mbalimbali kama kilimo, ufugaji, viwanda vidogo vya ushonaji na ujasiriamali wa aina tofauti ili kujiongezea kipato badala ya kutegemea muziki pekee.
“Wanamuziki tumekuwa na changamoto nyingi za maisha na hii inatokana na kujikita katika eneo moja la kufanya muziki tu bila ya kuchanganya na fursa nyingine ebu tuamke sasa tujikomboe serikali yetu sikivu ikiona jitihada zetu itatuunga mkono kwa kutupa maeneo ya kuanzisha kilimo na mtaji pia” alisema Joel.