*****************************
Klabu ya Simba imeendeleza kutoa tozi baada ya kufanikiwa kuinyuka Kagera Sugar mabao 2:0 kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unawafanya kuwatumia salamu watani wao wa jadi Yanga ambayo imetoka sare hapo jana dhidi ya Gwambina huku wakisubiri vita ya wenyewe kwa wenyewe hapo Jumamosi hii.
Huu ni mchezo wa pili mfululizo kwa Simba kushinda Uwanja wa Uhuru baada ya kuchezwa gwaride mara mbili mfululizo kwa msimu wa 2020/21.
Walianza kupoteza kwa kufungwa mbele ya Tanzania Prisons na wakafungwa na Ruvu Shooting mechi zote wakichapwa bao mojamoja.
Baada ya vipigo hivyo walianza kugawa dozi kwa mabao 5-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Uhuru, kisha leo wameibuka na ushinda wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Nahodha John Bocco dakika ya 42 leo amefunga penalti baada ya kukosa penalti ya kwanza aliyopiga msimu huu mbele ya Ruvu Shooting na bao la pili limefungwa na Said Ndemla dakika ya 45 kwa pasi ya Clatous Chama.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 19 ikiwa nafasi ya tatu ikiwa huku nafasi ya pili ikiwa kwa Azam FC wenye pointi 22 na Yanga ipo nafasi ya kwanza na pointi zake 23.
Kete inayofuata kwa Simba ambayo leo nyota wake mwenye mabao matatu Chris Mugalu aliingia kipindi cha pili baada ya kuwa nje kwenye mechi tatu kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ni dhidi ya Yanga, Novemba 7, Uwanja wa Mkapa.
Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema kuwa wanatambua mchezo wao ujao ni dhidi ya Yanga watapambana kupata ushindi.