………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk.Hassan Abbas,amesema kuwa maandalizi ya kuapishwa kwa Rais Mteule Dkt.John Magufuli yamekamilka na viongozi mbalimbali mashuhuri wa kitaifa na kimataifa wanatarajia kuhudhuria tukio hilo.
Akizungumza Waandishi wa Habari Jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri Dkt.Abass amesema kuwa wageni watakaohudhuria ni Rais wa Uganda Yoweri Museveni,Rais wa Comoro,Azali Assoumani,Rais wa Zimbambwe,Emmerson Mnangagwa pamoja na Mawaziri Wakuu na Makamu wa Rais wa Nchi mbalimbali.
Dkt.Abbas amesema kuwa tukio hilo la kihistoria ambalo ni mara ya kwanza kufanyika Mkoani Dodoma, pia litashuhudiwa na viongozi wenye hadhi ya juu Afrika akiwemo Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo na Mchungaji wa Kanisa la Church of All Nations lililopo Nigeria, Temitope Balogun Joshua maarufu kwa jina la TB Joshua.
” Jumla ya Mabalozi 83 wamedhibitisha kushiriki sherehe hizo ambapo Nchi ya Qatar itawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo”amesema Dkt.Abbas
Dk.Abass pia amesema kuwa sherehe hizo zitahudhuriwa na Marais wastaafu,Makamu wa Rais wastaafu na Mawaziri Wakuu
Aidha amesema kuwa kutakuwepo na Gwaride la heshima pia kutakuwa na wasanii mbalimbali akiwemo Nasib Abdul maarufu kwa jina la Diamond,AliKiba, Zuchu,Harmonize,Dulla Makabila,Sholomwamba na wengine.
Dkt.Abbas amesema kuwa utaratibu wa kuingia uwanjani, viongozi wote waliopewa kadi na vyama vya siasa, dini, majaji na watendaji wengine, yameandaliwa mabasi ya kuingiza wageni uwanjani na magari yao yatapark katika bustani ya chinangali.
Basi la kwanza litaondoka saa 12 na nusu asubuhi, viongozi wakuu wa kitaifa ambao wapo kwenye itifaki wao ndio magari yataingia uwanjani.
Hata hivyo amesema kuwa milango ya kuingia kwa wananchi watakaohudhuria tukio hilo yatakuwa wazi kuanzia saa kumi na mbili asubuhi wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma wanakaribishwa.