![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2020/11/03.jpg)
******************************************
Viongozi wa vyama tisa vya siasa vya upinzani Zanzibar vimetoa msimamo na kuunga mkono matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 ambao ulikuwa huru na haki na sasa vipo tayari kufanya kazi na rais wa Zanzibar dk.Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza na waandishi wa habari hapo katika ukumbi wa sheikh Idriss Abdull Wakil mjini Unguja,katibu wa umoja huo ambaye ni mgombeya wa urais kupitia Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir alisema ushindi wa mgombeya wa urais wa Zanzibar dk.Hussein Ali Mwinyi hauna mashaka ni wa kishindo ambao umeonesha kukidhi matarajio na matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.
”Umoja wa vyama tisa za upinzani vya siasa Zanzibar unatoa kauli ya kuunga mkono mgombeya wa urais wa Zanzibar dk.Hussein Ali Mwinyi ambaye ameibuka na ushindi na kuchaguliwa kuwa rais wa nane wa Zanzibar…tunamuunga mkono kwani ushindi wake umeonesha ndiyo mahitaji na matarajio ya wapiga kura wengi”alisema.
Aidha alisema uchaguzi umekwisha na huu ni wakati muafaka wa kushirikiana na rais dk.Mwinyi kujenga nchi na kutekeleza yale mambo mbali mbali aliyoyanadi kupitia ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi pamoja na ahadi zake kwa wapiga kura kutoka makundi mbali mbali.
Mapema katibu mkuu wa chama cha (UPDP) Hamad Mohamed Ibrahim akizungumza na waandishi wa habari alisema aliwapongeza wananchi wa Zanzibar walioshiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 kwa kufanya maamuzi sahihi ya kidemokrasia kumchaguwa dk.Hussein Ali Mwinyi kuwa rais wa Zanzibar.
Alisema uchaguzi ndiyo mchakato halali kwa njia ya kidemokrasia ya kupata viongozi wa kuongoza nchi ambapo maamuzi ya wapiga kura yanatakiwa kuheshimiwa.
”Tufike wakati viongozi wa vyama vya siasa tujenge utamaduni wa kuheshimu maamuzi ya wananchi ambao ndiyo wapiga kura na tuache tabia ya kukataa matokeo hatua ambayo inaweza kuliingiza taifa katika vurugu za kisiasa”alisema.
Aidha Naibu katibu mkuu wa chama cha (TLP) Hussein Juma Salum wamewataka wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa sababu uchaguzi umekwisha na hatua iliyobakiya ni kushirikiana na serikali iliopo madarakani kuleta maendeleo.
Aliwataka wanasiasa kuacha kuwadanganya wananchi na kuwapotezea muda kwa madai kwamba uchaguzi utarudiwa kutokana na shindikizo na matakwa ya mataifa ya nje.
”Si kweli wananchi wanachowaambiya wanasiasa kwamba uchaguzi utarudiwa kutokana na matakwa ya mataifa ya nje ambao wanadai kwamba uchaguzi hauku huru na haki…..Zanzibar ni nchi inayoongozwa kwa mujibu wa katiba na sheria zake”alisema.
Mapema akizungumza na gazeti hili kwa simu akielekea Dodoma kwa ajili ya kuhudhuria kuapishwa kwa rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli,Mwenyekiti wa chama cha Ada Tadea Juma Ali Khatib alisema wanaunga mkono hotuba ya rais DK.Hussein Ali Mwinyi katika siku ya kiapo cha utii na uaminifu ambayo imemtoa matumaini mapya kwa wananchi mbali mbali wa Zanzibar.
Aliwataka Wazanzibar kamwe wasikubali kurudi nyuma na kuingia katika mifarakano ya kisiasa kwa sababu athari zake ni kubwa ikiwemo vurugu na mchafuko ya kisiasa.
”Tumefanya uchaguzi na mshindi amepatikana ambaye ni dk.Hussein Ali Mwinyi….huu ni wakati wa kushikamana tujenga Zanzibar mpya yenye matumaini kwa sababu tunaona mwanga wa mafanikio”alisema.
Vyama vya siasa ambavyo vinaunda Umoja wa vyama vya upinzani vinavyoyakubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 na kumuunga mkonorais dk.Hussein Ali Mwinyi ni AAFP,ADA-TADEA,ADC,DEMOKRASIA MAKINI,NLD,SAU, pamoja na TLP na UPDP.