Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk.Bashiru Ali,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya kuongeza muda wa uchukuahi fomu za kuwania Uspika na Unaibu Spika ,Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya wa Manispaa na Majiji jijini Dodma
…………………………………………………………………….
Na Alex Sonna, Dodoma
Chama cha Mapinduzi(CCM), kimeongeza muda wa uchukuaji fomu za kuwania Uspika, Unaibu Spika, Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya wa Manispaa na Majiji.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk.Bashiru Ali, amesema kwa nafasi ya Uspika fomu zitaendelea kutolewa na kurejeshwa hadi kesho saa 10 jioni.
Aidha, alisema kwa Wenyeviti na Mameya mwisho utakuwa Novemba 5, mwaka huu ili kupanua demokrasia na kupata fursa ya kuchambua na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa fedha na mali za umma.
Aidha, amesema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM itafanya kikao chake Novemba 6, mwaka huu Jijini Dodoma kwa ajili ya kupitisha majina ya walioomba Uspika wa bunge na kupokea taarifa ya awali ya utekelezaji wa mpango wa CCM wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Agenda ya pili ni kupitia majina ya wanachama waliomba nafasi ya uspika katika baraza la wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na muda umeongezwa kwa uspika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uwakilishi zoezi limekamilika na vikao vya awali vimefanyika,”amesema.
Amesema Kamati maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa imeshaketi na kutoa mapendekezo yatakayojadiliwa katika kikao cha sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kesho kuhusu Uspika wa Baraza la Wawakilishi ambapo wamejitokeza watano akiwemo aliyekuwa Spika Zuberi Ali Maulid.
Hadi leo saa 10 jioni wanachama watatu waliokuwa wamejitokeza kuchukua fomu kuwania Uspika wa Bunge ambapo kati yao mmoja ni nafasi ya Unaibu Spika.
Waliojitokeza katika nafasi ya Uspika ni Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai, na mwanachama kutoka Mkoa wa Songwe Stamina Mdolo huku nafasi ya Unaibu Spika ni Dk.Tulia Ackson.