**************************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
JUMLA ya wagonjwa 5 sawa na asilimia 2.4 kati watu 203 waliobainika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu walioibuliwa kupitia kampeni ya uelimishaji na uibuaji ya ugonjwa huo inayofanywa na hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, wamepoteza maisha katika kipindi cha robo ya tatu ya Julai hadi Septemba 2020 wilayani Tunduru.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema hayo jana katika kampeni ya uelimishaji na upimaji wa kifua kikuu kwa watu na makundi mbalimbali ikiwemo mama lishe na waendesha boda boda iliyofanyika katika hospitali ya wilaya Tunduru mjini.
Alisema, idadi hiyo ya vifo ni ongezeko la mtu mmoja ikilinganisha na watu 4 walipoteza maisha mwaka 2019 kati ya 145 waliokutwa na maradhi hayo kupitia kampeni hiyo.
Alisema, kwa upande wa watoto walio chini ya umri wa miaka 15 waliokutwa na kifua kikuu mwaka 2020 ni 75 sawa na asilimia 36.9 na mwaka 2019 waliokutwa na maambukizi ya Tb ni 25 sawa na silimia 17.2.
Aidha alisema,mwaka 2019 jumla ya wahisiwa(waliofanyiwa uchunguzi)wa ugonjwa wa kifua kikuu 1654 waliokutwa na vimelea vya ugonjwa huo ni 145 na hadi kufikia mwezi Septemba 2020 wahisiwa walikuwa 4073 kati yao 203 walipatikana na maambukizi.
Baadhi ya wananchi wameishukuru serikali kupitia wizara ya Afya kwa mpango wake wa kufanya kampeni ya kuibua wahisiwa wa ugonjwa wa kifua kikuu ambao umesaidia sana kuokoa maisha ya wananchi wengi.
Wakizungumza jana katika zoezi la kampeni ya uhamasishaji na uelemishaji kuhusu ugonjwa huo iliyofanyika katika Hospitali ya wilaya Tunduru walisema, mpango huo umewezesha kuibuliwa kwa wananchi wengi wenye ugonjwa huo majumbani ambao hawakufahamu maradhi yanayowasumbua kwa muda mrefu.
Hata hivyo,wameomba kuongezwa dawa ya Isoniazid ambayo ni muhimu kwa wagonjwa wa TB na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma vilivyopo jirani na maeneo yao ili watu wanaobainika kupata ugonjwa huo waweze kupata tiba sahihi na kwa wakati badala ya kwenda mbali ili kuepuka usumbufu.
Habiba Yasin,Abdul Hassan na Juma Makumbusya walisema, kampeni inayofanywa na hospitali ya wilaya ya Tunduru chini ya kitengo cha kifua kikuu na ukoma, itaokoa maisha ya baadhi ya watu wanaogua ugonjwa huo kwa muda mrefu hasa katika vijiji vilivyopo mpakani mwa wilaya ya Tunduru na nchi jirani ya Msumbiji
Juma Makumbusya mkazi wa kijiji cha Kitanda wilayani humo alisema, elimu inayotolewa na kitengo cha kifua kikuu imewezesha wazazi kujua dalili za kifua kikuu kwa watoto wadogo ikilinganisha nah apo nyuma ambapo hawakuwa na uwelewa kuhusu dalili za ugonjwa huo hasa kwa watoto.
Alisema, baadhi ya wazazi wamepoteza watoto wao kwa kukosa uwelewa wa kifua kikuu na suala zima la afya,kwa hiyo kama serikali itaendelea na kampeni za uelimishaji watanzania wengi watachukua taadhari ya kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Alisema, wazazi wengi hawafahamu kama mtoto kulia mara kwa mara ni kati ya dalili za kifua kikuu badala yake waliamini kulia kwa mtoto kunatokana na kupewa jina ambalo halipendi au halipo katika ukoo wao.