*********************************************
Na Emmanuel J. Shilatu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu Tanzania upande wa ngazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aambapo idadi ya waliopiga kura ilikuwa kura 15,091,950 ambapo kura halali ni 14,830,195 ambapo Mhe. John Pombe Magufuli wa CCM amepata kura 12,516,252 sawa na 84.4% huku anayemfuatia kwa mbaali akiambulia kura 1,933,271 sawa na 13.04%.
Nampenda kuungana na mamilioni ya Watanzania kumpongeza Mhe. Dk. John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi kuchaguliwa tena kwa awamu ya pili kuwa Rais wa Tanzania.
Ni ushindi wa kihistoria tangu kuanza mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995. Historia inaonyesha aliyewahi kupata kura nyingi tangu mfumo wa vyama vingi uanze nchini alikuwa Hayati Benjamin Mkapa kwenye uchaguzi Mkuu mwaka 2000 ambapo alipata kura milioni 5.9 sawa na asilimia 71.7 ambapo mwaka 2020 Dk. Magufuli amevunja rekodi hiyo na zote kwa kupata kura zaidi ya milioni 12.5 sawa na asilimia 84.4 .
Ni ushindi mnono ulioutoa shimoni CCM ambayo kura zake zilikuwa zikipungua kila mwaka wa uchaguzi. Ambapo mwaka 2005 Mzee Jakaya Kikwete alipata ushindi 80.3%, mwaka 2010 kura zikapunguka akapata 63.8%. Uchaguzi wa mwaka 2015 uliomuingiza Dk. Magufuli madarakani CCM ilizidi kuporomoka kwa kupata ushindi wa 58.6%. Mwaka huu 2020 Mgombea wa CCM na Mwenyekiti CCM Taifa Dk. Magufuli amepata ushindi wa kishindo na wa kihistoria wa asilimia 84.4 , sitakosea nikisema Mwamba Dk. Magufuli ameitoa CCM shimoni na kuirudisha kwenye ramani.
Ni Watanzania ndio walioamua kuchagua kazi, historia, amani, haki, usawa na maendeleo ambayo wameona mwangaza wa upatikanaji wake kupitia Rais Magufuli, kupitia CCM kutoana na kuridhishwa na sera, ilani ya CCM.
Imani ya CCM imerudi kwa jamii kutokana na uadilifu, uzalendo, uchapa kazi, ufuatiliaji na ucha Mungu alionao Rais Magufuli ambaye amejitolea kwa dhati kabisa kuwa sadaka ya Watanzania ya kuwaletea maendeleo ambapo leo hii sisi Watanzania tunasomeka Duniani kote tumeingia kwenye nchi zenye uchumi wa kati. Hakika, Rais Magufuli ni jembe.
Ni ushindi uliojaa fundisho kwa wale wote wasiotutakia mema, wasiopenda amani tuliyonayo, wasiopenda maendeleo tunayoanza kuyaona kupitia kiongozi jasiri na shupavu, Dk. Magufuli.
Ni ushindi wa kishindo, fundisho na salaam Duniani kote kuwa tunaridhishwa na kuunga mkono mambo yote yanayofanywa na Rais Magufuli ya ukombozi wa kiuchumi kwani Tanzania ni tajiri na tunaweza kujikomboa sisi wenyewe.
Ni ushindi uliojaa fundisho kwa wale wanaotaka kutugawa ili watuvuruge kuwa Watanzania wa leo wameelimika sana wamejaa umoja, mshikamano na uzalendo kwa Taifa lao tukufu la Tanzania na wapo tayari kuilinda Tanzania na Rais Magufuli kwa gharama yeyote ile.
Kwenye uchaguzi wowote ule kuna kushinda na kushindwa, ni muhimu Wanasiasa na wagombea kuheshimu maamuzi ya Watanzania kama ambavyo zaidi ya Wagombea 9 wa nafasi ya Urais walivyokubali wameshindwa kihalali kabisa kwani muda wa uchaguzi na siasa umekwisha.
Ni muhimu kutambua pia kuna maisha baada ya uchaguzi. Amani tuliyonayo, maendeleo tuliyonayo, Tanzania tuliyonayo ni muhimu zaidi kuliko kitu chochote kile. Tuitunze Tanzania yetu kwani hatuna Tanzania nyingine.
Narudia tena kumpongeza Rais Magufuli kwa ushindi mnono, wa kihistoria na wa fundisho alioupata.