******************************************
RAIS Mteule ya Zanzibar DK. Hussein Ali Mwinyi leo anatarajiwa kuapishwa na kuwa Rais wa awamu ya nane wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Hafla ya kuapishwa Rais mteule huyo itafanyika katika viwanja vya Amani Abeid Karume mjini Unguja, na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DK. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar anayemaliza muda wake, DK. Ali Mohammed Shein.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar DK. Abdulah Juma Sadala alisema mabalozi zaidi ya 26 wa ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika ghafla hiyo.
Alisema, wageni wengine wanaotarajiwa kushiriki katika sherehe hizo ni pamoja na vyama rafiki vya siasa kutona nchi mbali mbali kama vile, Namibia, Msumbiji, Uganda, Ghana, Kenya, China, Moroco, DRC Kongo, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Hata hivyo DK. Mabodi aliwataka wananchi mbali mbali wa Zanzibar na nje ya Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Amani kushuhudia kuapishwa kwa Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar.
"Nakuombeni sana mje kwa wingi wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi mje kushuhudia kile ambacho mlikiamua katika chumba cha kupigia kura Oktoba 28," alisema.
Aidha aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kuweza kumpa ushindi wa kishindo mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi DK. Hussein Ali Mwinyi na kufanya apate ushindi wa asilimia 76 ushindi ambao ni wa kihistoria.
Alisema, wananchi wa Zanzibar wameonyesha kwa kiasi kikubwa imani yao juu ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi wa mwaka huu na kuahidi kuwa Chama hicho kitashirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo ya nchi.
Aidha aliwashukuru pia wananchi hao wa Zanzibar kwa kuwachagua kwa wingi Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Chama cha Mapinduzi na kukifanya Chama hicho kuchukua jumla ya Majimbo 45 kati ya Majimbo 50 yaliyopo Unguja na Pemba.
Akizungumzia siri ya ushindi wa CCM, alisema ni uwepo wa sera imara,kampeni za kisayansi za kuwafuata wananchi katika makaazi yao kuwaeleza namna watakavyotatuliwa changamoto zao sambamba na utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Alisema CCM imeendelea kuwa muumini mkubwa wa kulinda amani na utulivu nchini ili wananchi wapate uhuru wa kufanya shughuli zao za maendeleo kwa utulivu.