Na John Walter-Babati
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Babati Vijijini John Nchimbi amemkabidhi cheti cha Utambuzi Mbunge wa Jimbo hilo Daniel Sillo pamoja na Madiwani 25 wa Chama cha Mapinduzi waliochaguliwa .
Msimamizi huyo ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati amewataka Madiwani kutambua kuwa wao ni sauti ya wananchi hivyo wakafanye kazi walizowaahidi.
Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho leo Oktoba 30, 2020 katika ofisi za Halmashauri za wilaya ya Babati Mbunge huyo amesema atashirikiana na wanachi katika kutatua changamoto zilizopo za Maji,Umeme pamoja na kuongeza vituo vya afya ili kusogeza huduma karibu.
Amesema kazi iliyopo kwa sasa baada ya Uchaguzi mkuu kumalizika ni kuwahudumia wananchi wa Babati akishirikiana na Madiwani katika kata 25 za Jimbo hilo.
Katika upande mwingine Sillo ameahidi kushirikiana na vijana kwa kuwashauri kujiunga kwenye vikundi ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia mitaji isiyokuwa na riba watakayopatiwa kutoka Halmashauri.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Babati Vijijini Filbert Mdaki amewapongeza wasimamizi wa uchaguzi ambao wamesimamia haki na kufanya uchaguzi kuwa wa utulivu na amani katika Jimbo hilo.
Jimbo la Babati Vijiji lina jumla ya kata 25 na zote zimechukuliwa na Chama cha Mapinduzi.