MGOMBE Urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC Taifa Hamad Rashid Mohamed, akitumbukiza kura yake katika moja ya masanduku ya kura yaliyowekwa na tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC, katika kituo cha kupigia kura Fidel Casro Wawi jimbo la Wawi.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia chama cha wananchi CUF Mussa Haji Kombo, akitumbukiza kura yake katika moja ya masanduku ya kupigia kura yaliyowekwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)katika kituo cha Wara kilimo Mchaomanne jimbo la Wawi.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia chama cha wananchi CUF Mussa Haji Kombo, akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari Tanzania, mara baada ya kupiga kura kituo cha Wara kilimo Mchaomanne jimbo la Wawi. MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia chama cha Wakulima Tanzania (AFP) Said Soud Said, akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari Tanzania, mara baada ya kupiga kura kituo cha Skuli ya Wawi Jimbo la Wawi Wilaya ya Chake Chake.
*****************************************
NA MWANDISHI WETU, PEMBA
ZOEZI la upigaji kura kisiwani Pemba, limeripotiwa kwenda vyema, huku vituo navyo vikifugulia kwa wakati na vifaa kuripotiwa kufika kwa wakati.
Waandishi wetu waliotembelea vituo mbali mbali, walisema wananchi wengi wao, walifika kwenye vituo hivyo baina ya saa 11:55 na saa 12:00 asubuhi ingawa wengine walikwenda chini ya hapo.
Wakizungumza na waandishi wetu, wapiga kura hao walisema vituo vilifunguliwa kwa wakati uliopangwa na tayari ilipofika majira ya saa 1:00 asubuhi, vilianza kazi kwa kasi.
Walisema, hata watendaji wa Tume za Uchaguzi ya Zanzibar ZEC na ile ya taifa ya NEC, wamekuwa na uharaka wa kutoa huduma kwa wananchi wanaoingia vituoni, jambo ambalo linaweza kusababisha hadi ikifika saa 9:00 huwenda wakawa wameshamalizika.
Ali Khamis Makame ambae ni mpiga kura kwa mara ya kwanza, akiwa kituo cha Fidel- Castro jimbo la Wawi alisema, hali iko shuwari.
“Mimi nilitoka nyumbani nikiwa na woga, lakini hadi nafika kituoni sijazuiwa na wala sikutumia muda mrefu kituoni, nawaomba wengine waje,’’alisema.
Aisha Khamis Haji miaka 60, alisema kati ya chaguzi zote alizowahi kushiriki, wa mwaka huu 2020, umekuwa bora zaidi kwa kule kuimarisha ulinzi.
“Jengine ambalo naliona ni zuri liliowekwa na tume zetu kwa sisi wazee, walemavu, wenye watoto wachanga na wajawazito tumewekewa foleni yetu, hili linapunguza machungu,’’alieleza.
Akizungumza kwenye eneo hilo, Waziri wa Nchi afisi ya Makamu wa Pili wa rais Mohamed Aboud Mohamed, alipongeza kasi ya watendaji wa Tume.
Alisema zoezi hilo huwenda likalaini mno, jambalo ambalo litawapa nafasi na fursa ya wananchi wengi kupiga kura.
“Zoezi liko rahisi na laini mno, na inaonekana kwa uchaguzi huu wa mwaka 2020, wananchi wamepata muamko mkubwa, maana leo kila kituo unachopita unakuta watu wengi,’’alieleza.
Wananchi wa Jimbo la Chake Chake wa vituo vya skuli ya Michakaini na Mdungu, walisema utaratibu wa kuweka foleni za wanawake na wanaume mbali mbali ni jambo jema.
Khamis Nahoda Juma (55) na Fatma Haji Khamis (20) waliokuwa vituo vya skuli ya msingi Michakaini walisema, kama chaguzi zote zingekuwa kama wa mwaka huu, kusingekuwa na lawama.
Hamad Juma Hamad (19) na Asha Himid Mmanga wa vituo vya Micheweni Jimbo la Micheweni, waliwataka wenzao ambao wana hofu kufika vituoni.
Omar Hamad Jabu (30) na Fatma Khamis Muhidini (50) wa kituo cha skuli ya Jadida Jimbo la Wete, wakizungumza na vyombo vya habari, walisema zoezi hilo liko vyema na wala halijatawaliwa na vurugu.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Ole kwa tiketi ya UMMA, Maryam Saleh Juma alisema, hadi majira ya saa 04:15 asubuhi zoezi hilo kwenye vituo skuli ya Vitongoji, Vikunguni ‘A’, Ole, Mbuzini, Laureat, Uwandani, Vikunguni ‘B’, mawakala wao hawakuruhusiwa kuingia.
Alisema ni vituo vya skuli ya Vitongoji pekee, ambapo humo ndio Tume ya Taifa ya NEC imewaruhusu kuwapokea na kuwajazisha fomu mawakala wao.
“Kwa upande wetu sisi CHAUMMA tunasema zoezi la upigaji kura ni gumu na limeshaingo dosari, licha ya kuwa wameshaiandikia barua NEC, lakini hadi saa 4:15 asubuhi hawajatujibu na zoezi la kura linaendelea,’’alifafanua.
Mgombea uwakilishi wa Jimbo la Mtambile kwa tiketi ya CUF Asha Said Suleiman alisema, zoezi ni zuri na vituo vilifunguliwa kwa wakati uliopangwa.
“Mimi mwenyewe hadi saa 3:50 asubuhi sijapiga kura, lakini nimesharidhika nalo maana, nilipofika skuli ya Mizingani hapa nimelifurahia mno na jinsi ulinzi ulivyoimarishwa ,’’alieleza.
Mgombea uwakilishi jimbo la Mkoani kwa tiketi ya ACT-Wazalendo Seif Khamis Mohamed, alisema zipo baadhi ya kasoro alizoziona wakati anavitembelea vituo kadhaa.
Alisema kasoro hiyo ni kuzungurushwa wapiga kura, baada ya kumaliza kupiga kura ya Zanzibar, na wapo wanaowahi kutoka nje kabla ya kupiga kura ya Muungano.
Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADC Hamad Rashid Mohamed, alisema ulinzi jinsi ulivyoimrishwa umewasababisha wananchi kujitokeza kwa wingi.
“Ulinzi uliimarishwa tokea usiku wa Oktoba 26, ndio maana hilo limesababisha kila mmoja kutumia haki yake ya kumchagua kiongozi amtakae,’’alisema.
Nae mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya NRA, Khamis Faki Mgau, amesema zoezi la upigaji kura limevuta hisia ya wananchi kadhaa, kwa kule kuwepo na utaratibu mzuri uliowekwa na tume.
“Mimi nimeridhika na upigaji kura hadi sasa, na tayari nimeshapiga kura na wala sijaona usumbufu wowote, na ambao bado hawajafika, wajitokeze watumie haki yao,’’alisema.
Nae mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya AAFP, Said Soud Said, alisema kutokana na uchaguzi kuwa huru, atayapokea matokeo yatakavyokuja.
“Matumaini yangu ni kushinda maana hichi ni chama cha wakulima, lakini upepo ukigeuka nami nitampongeza mshindi,’’alieleza.
Hata hivyo mgombea huyo, amewataka wananchi kuendelea kurudi nyumbani, mara baada ya kumaliza zoezi la upigaji kura, ili kulinda amani iliyopo nchini.
Nae Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha wananchi CUF Mussa Haji Kombo, alisema ameridhishwa na zoezi hilo kwa kiwango kikubwa.
“Zoezi ni zuri mno, maana tume zetu zimeweka utaratibu ambao hauna usumbufu, sasa kilichobakia ni kwa wananchi kutumia haki yao,’’alieleza.
Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla alisema, serikali ya mkao itaendelea kuimarisha ulinzi, ili kila mwenye haki ya kupiga kura, aitimize.
Akizungumza kwa njia ya simu Mgombea uwakilishi Jimbo la Chambani kwa tiketi ya CCM Bahati Khamis Kombo, alisema tayari ameshavitembelea vituo vya kupigia kura kama vile Dodo, Chambani na Ukutini huku hali ikiripotiwa kuwa shuwari.
“Vituoni hakuna fujo wala usumbufu, ukifika unaangalia jina lako na namba ya kituo chako, kisha kama mwanamke unakaa walipo wenzako na kutumia haki yako,’’alieleza.
Hata hivyo mgombea ubunge Jimbo la Chake Chake kwa tiketi ya CHADEMA Rukia Abuu Mohamed, hakuwa tayari kusema lolote wakati wa zoezi hilo likiendelea.
Baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC, ambao walitaka majina yao yasitajwe kwa vile sio wasemaje, walisema zoezi hilo linakwenda vyema.
Walisema kwa vile walilala vituoni tokea Oktoba 27, hivyo walipanga vitendea kazi vyao, mapema na ilipofika saa 1:00 asubuhi kazi lilianza.
Hata hivyo wasimamizi wa uchaguzi wa vituo kadhaa walikataa kutoa ushirikiano na waandishi wa habari, kama ilivyozoeleka chaguzi zilizopita.