Na. Lilian Shembilu – MAELEZO
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Wilson Mahera amewaapisha mawakala wa vyama vya siasa 14 ambapo Chama cha ACT-Wazalendo hakina mwakilishi wa uwakala, hivyo kufanya idadi ya Vyama vya siasa vitakavyogombea nafasi ya urais tarehe 28 Oktoba 2020 kufikia 15.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt.Wilson Mahera amesema mawakala wa wagombea wa nafasi ya urais ni wawakilishi walioteuliwa na chama baada ya kupata ridhaa ya wagombea wao.
“Wakala wa kujumlisha kura ni mwakilishi aliyeteuliwa na Chama baada ya kupata ridhaa ya mgombea, kwahiyo mliopo humu ndani mmeteuliwa na vyama vyenu baada ya ridhaa ya mgombea, hongereni sana” amesema Dkt. Mahera.
Dkt. Mahera amewaeleza wajibu na majukumu ya mawakala kuwa ni kushuhudia ujumlishaji wa kura za urais, kulinda maslahi ya mgombea na wagombea kwa kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni zinafuatwa wakati wa kujumlisha matokeo ya uchaguzi na kanuni hizo za sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 na kuzingatia pia katiba ya nchi, vilevile mawakala wana wajibu wa kusaini fomu ya matokeo ya uchaguzi.
“Si kuhesabu kura tu bali kufuata sheria na kanuni zote za wakala na ukienda ndivyo sivyo utawajibika kama sheria inavyosema” amesema Dkt. Mahera.
Akizungumza katika kikao hicho mwanasheria wa Serikali Bi.Rose Chilongozi aliwaasa mawakala wote kuhakikisha wanasimamia kiapo walichoapa na wajue kuwa wakivujisha siri ambazo hawakuambiwa wazitoe na kwamba zitatolewa na wahusika hilo ni kosa la jinai.