Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akizungumza kaika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye uwanja wa maegesho ya magari wa Nachingwea,
Wananchi wa Nachingwea wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa maengesho ya magari, Nachingwea,
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli Oktoba 27, 2020 amezungumza na wananchi wa Nachingwea kwa njia ya simu katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa maegesho ya magari, Nachingwea. Pichani, Mheshimiwa Majaliwa akiwa amesogeza simu kwenye vipaaza sauti ili kuwawezesha wananchi kusikia sauti ya Rais Dkt. Magufuli.
.………………………………………………………………………..
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amepiga simu na kuwaomba wakazi wa Nachingwea wampe kura za ndiyo hapo kesho watakapoenda kupiga kura.
Kesho, (Jumatano, Oktoba 28, 2020) ni siku ya uchaguzi mkuu hapa nchini ambapo Watanzania watapata nafasi ya kumchagua Rais, Wabunge na madiwani.
Dkt. Magufuli ameongea nao leo mchana (Jumanne, Oktoba 27, 2020) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Nachingwea kupitia simu aliyompigia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Boma katika mkutano uliofanyika viwanja vya Bomani kwenye mji mdogo wa Nachingwea, mkoani Lindi.
Mheshimiwa Majaliwa leo amehitimisha mikutano ya kampeni ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Nachingwea kupitia CCM, Dkt. Amandus Chinguile na wagombea udiwani wa kata za wilaya hiyo.
“Ninawasalimu sana wana-Nachingwea. Zile changamoto za zao la korosho, ninazijua; zile changamoto za barabara ninazijua na yote hayo tumeyapanga kwenye Ilani yetu. Nilitamani nifike huko lakini nimemtuma Waziri Mkuu wangu mpendwa aje kuniombea kura, yote atakayoyasema ni ya kwangu. Baada ya uchaguzi, nitakuja kuwaona.”
“Nawaombeni kura zenu nyingi, nawaomba mumchague mbunge wa CCM na madiwani wa CCM ili tufanye nao kazi. Nataka Nachingwea ibadilike, zile barabara zote tutazijenga kama tulivyoahidi kwenye ilani yetu,” amesema.
Baada ya Rais Dk. Magufuli kuzungumza na wananchi hao, Mheshimiwa Majaliwa aliwasisitiza wakazi hao wahakikishe kesho wanapiga kura zote za ndiyo kwa mgombea urais, wabunge na madiwani wa CCM ili wapate ushindi wa kishindo.
“Kesho asubuhi, kila mmoja na kadi yake, nenda kapige kura. Wako waliojipanga kununua kadi za wapigakura ili kutunyima ushindi. Kura yako ina thamani sana kuliko hiyo elfu tano atakayokupa. Usikubali kupoteza kura yako.”
Wakati huohuo, mbunge mteule wa jimbo la Mtama, Bw. Nape Nnauye alipopewa nafasi kumuombea kura Dkt. Magufuli alisema ana imani kwamba ushindi wa CCM uko dhahiri kwani hapo Nachingwea wakazi wake ni karibu 100,000 lakini wanaCCM peke yake ni 86,000.
“Hawa wanataka kushindana na CCM, sasa hao watashindaje? Kati ya majimbo zaidi ya 200 hapa nchini, tayari tuna majimbo 28 ambayo wagombea wake wamepita bila kupingwa. Tukienda kwenye urais, tuna wapiga kura milioni 29 na kati yao, milioni 18 ni wanaCCM. Je bado wana nafasi ya kushinda? Watapitia wapi?” alihoji.
Aliwataka wakazi hao waache ushabiki wa kisiasa na wajifunze kutoka nchi jirani ambayo wananchi wake walipata maafa baada ya uchaguzi na wagombea wakabakia na makundi.