**********************************
NA FARIDA SAIDY,MOROGORO
Serikali Mkoani Morogoro imewataka wananchi mkoani humo kujiepusha na makundi yoyote yenye viashiria vya uvunjifu wa amani na kufanya vurugu kwenye vituo vya kupigia kura siku ya oktoba 28 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo amesema Mkoa wa Morogoro umejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama katika vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo Ole Sanare amewataka wananchi wote waliojiandikisha kupigia kura kwenda kupiga kura siku ya tarehe 28 oktoba 2020 ili kutimiza takwa la kikatiba la kuchagua madiwani, wabunge na Rais, ambapo zoezi hilo hutokea mara moja ndani ya miaka mitano.
Mkoa wa Morogoro una una jumla ya Majimbo 11,kata 214,huku vituo vya kupigia kura vikiwa 4,774 na waliojiandikisha katika daftari la kudumu la kupiga kura ni 1,623,629.