Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma George Bisani katikati akikagua moja ya ghala la kuhifadhia korosho zilizozalishwa katika msimu wa 2020 kabla ya kuanza mnada wa kwanza wa zao hilo uliofanyika kijiji cha Muhesi ambapo zaidi ya tani 1902 zimekusanywa hadi kufikia jana hata hivyo wakulima wa zao hilo wamekaaa kuuza korosho zao kutokana na bei ndogo iliyotolewa na wafanyabiashara,kushoto Mkurugenzi wa kampuni ya Yuha Co Ltd inayojishughulisha na utunzaji wa maghala Khaji Thabiti,
Picha na Muhidin Amri
…………………………………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
WAKULIMA wa korosho mkoani Ruvuma, wamegoma kuuza korosho zao katika mnada wa kwanza katika msimu 2020 uliofanyika katika kijiji cha Muhesi kufuatia wanunuzi waliojitokeza kutangaza kununua zao hilo kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya uzalishaji.
Katika mnada huo makampuni mawili yalijitokeza kununua korosho kwa bei kati ya shilingi 2180 hadi shilingi 2350 bei ambayo ni kidogo mno ikilinganisha na bei ya korosho zilizouzwa ya shilingi 2700 katika mikoa jirani ya Lindi na Mtwara.
Wakizungumza jana mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro wakulima hao walisema, bei iliyotangazwa na wanunuzi ni ndogo kwa hiyo hawako tayari kuuza hadi pale itakapotangazwa bei mzuri katika mnada wa pili utakaofanyika tarehe 29 Oktoba.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru (Tamcu) Ltd Hashim Mbalabala alisema, haiwezekani hata kidogo wao kama wakulima kuuza korosho kwa bei ya kutupa na kuwataka wanunuzi kuwahurumia wakulima ambao wamekuwa wanaangaika kufanya shughuli zao katika mazingira magumu na gharama kubwa.
Alisema, bei iliyoletwa na wanunuzi hao kimsingi haina faida kwa wakulima, kwa hiyo hakuna mkulima aliyekubali kuuza korosho kwa bei ndogo na kuwataka wanunuzi hao kujitafakari kama kweli wana lengo la kununua.
Mkulima ambaye ni mwanachama wa Namiungo Amcos Juma Bakari alisema, bei iliyotolewa na wanunuzi imdewavunja nguvu wakulima kwani hailingani hata kidogo na gharama za kuandaa mashamba hadi kufikia hatua ya kuuza.
Alisema, bora korosho kukaa nazo ndani kuliko kuuza kwa bei ya chini ambayo kimsingi kama wangekubali baadhi ya wakulima wangejikuta matatani kwa kushindwa kulipa pembejeo walizokopa kwa wafanya biashara.
Kwa upande wake muneja mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru Tamcu Imani Kalembo alisema, hadi kufikia jana(juzi) zaidi ya tani 1902 ziliingizwa katika mnada wa kwanza wa korosho msimu 2020.
Kwa mujibu wa Kalembo,licha ya changamoto ziliojitokeza hata hivyo wanategemea kupata korosho nyingi kutoka katika vyama vya msingi vya ushirika ambapo wakulima wanaendelea kupeleka korosho zao kwa ajili ya kuuza katika minada inayofuata.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro ameiagiza katika minada inayofuata wanunuzi kuleta bei nzuri ambayo itawanufaisha wakulima kama ilivyo katika minada iliyofanyika katika mikoa jirani ya Lindi na Mtwara ambapo bei ya korosho ilikuwa kati ya shilingi 2500 hadi 2700.
Alisema, kama wanunuzi hawatakubali kuleta bei nzuri basi serikali ya wilaya inaweza kuweka utaratibu mwingine utaratibu mwingine wa kuuza korosho ambao utawasaidia sana wakulima wa wilaya hiyo badala ya kuendelea na wafanya biashara wababaishaji ambao wana lengo la kurudisha nyuma juhudi za wakulima.
“kimsingi bei zilizoletwa na wanunuzi katika mnada wetu wa leo sio rafiki kabisa kwa mkulima na hazileti mahusiano mazuri kati yao na wakulima, hizi sio bei sahihi hata kidogo ni lazima wanunuzi wajitafakari kama kweli wana nia ya kununua korosho zinazolimwa katika wilaya yetu”alisema.
Aidha Mkuu wa wilaya, amepiga marufuku wafanyabiashara kwenda kununua korosho katika vyama vya msingi vya ushirika, badala yake kuelekeza wafanya biashara wote kununua korosho ambazo zimeingizwa katika maghala maalum yaliyoteuliwa.