Mkurugenzi wa Uchaguzi jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini Gasper Balyomi, akiongea jana na wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika mafunzo ya siku mbili ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya wiki hii,kushoto ni mkufunzi wa mafunzo hayo Hodari Patrick,
Baadhi ya wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoka jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini wakimsikiliza Mkurugenzi wa Uchaguzi Gasper Balyomi(hayupo pichani)wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo namna ya kuzitambua na kuzingatia sheria zilizowekwa na tum ya taifa ya uchaguzi.
Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi majimbo ya Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini wakila kiapo cha kutunza siri za uchaguzi jana wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo na kufahamu sheria mbalimbali za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Picha zote na Mpiga Picha Wetu
……………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
MKURUGENZI wa Uchaguzi katika jimbo la Tunduru kusini na Tunduru kaskazini mkoani Ruvuma Gasper Balyomi amewataka wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,kuzingatia viapo vyao pamoja na kujiepusha na tabia ya ulevi wakati wote wa zoezi la upigaji na kuhesabu kura na taratibu na sheria zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Balyomi,ametoa kauli jana wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Sky Way mjini hapa.
Alisema, hawatakiwi kufanya mambo yote yaliyokatazwa na tume ya taifa ya uchaguzi ikiwemo kuingia na simu katika chumba cha kuhesabiwa kura,ulevi inayoweza kusababisha fujo na kuathiri zoezi zima la uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Amewataka kufuata yote waliyofundishwa na tume ya taifa ya uchaguzi na kutofanya kazi kinyume na maelekezo ya tume ya taifa na iwapo itabainika msimamizi wa kituo na msimamizi msaidizi kwenda kinyume,wataondolewa katika vituo na kutafutwa mtu mwingine.
Aidha,amewataka kujiepusha na itikadi za vyama na kupendelea wagombea, badala yake kwenda kutenda haki kwa kila chama wakati wote wa zoezi zima la uchaguzi ili kuepusha vurugu na malalamiko.
Balyomi ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru,amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kwenda kutekeleza vema yale waliofundishwa ikiwemo suala la uadilifu,weledi na kuepuka aina yoyote ya upendeleo kwa vyama vya siasa na wagombea.
Alisema, matumaini ya tume ya uchaguzi kwamba baada ya kupata mafunzo hayo watakwenda kutekeleza majukumu waliyopewa na tume hiyo kwa juhudi,maarifa, na kushirikiana na wadau wengine wa ucahguzi huo.
Aidha, amesisitiza suala zima la kuzingatia uadilifu wakati wa mchakato wa uchaguzi na kuwasisitiza kufuata kanuni na sheria za uchaguzi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Allen Chukwa, ameishukuru tume ya taifa ya uchaguzi kwa kutoa mafunzo ambayo yatawapa uwezo wa kutekeleza majukumu yao katika zoezi zima la ucahguzi mkuu wa mwaka huu.
Amewaasa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wa uchaguzi, kwenda kutenda haki kwa wagombea na vyama vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi mkuu ili kuepuka malalamiko yasio ya lazima.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Hodari Patrick alisema, katika mafunzo hayo wasimamizi wa vituo na wasimamizi wa uchaguzi wanafundishwa namna ya kusimamizia vizuri mchakato wa uchaguzi,kuhesabu kura pamoja na majukumu mengine yaliyolewa na tume ya Taifa ya uchaguzi.
Hodari alisema, ni matumaini kwamba mafunzo hayo yatawasaidia sana kwenda kufanya kazi kwa kufuata maelekezo ya tume na msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kushirikiana na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo.