…………………………………………………………………………..
Na. Lillian Shirima MAELEZO
Oktoba 28, 2020 Watanzania watapiga kura ya kumchagua kiongozi atakayeongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Tangu kuzinduliwa rasmi kwa kampeni za uchaguzi Agosti 26, mwaka huu mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza umuhimu wa kutunza na kulinda tunu ya amani tuliyonayo akisema yapo maisha baada ya uchaguzi.
Akiwa mkoani Kilimanjaro katika Jimbo la Hai, Rais Magufuli aliongea na wananchi waliohudhuria mkutano wake wa kampeni uliofanyika Bomang’ombe na kusisitiza juu ya suala la amani na utulivu huku akiwashukuru viongozi wa dini kwa kuwakumbusha wananchi umuhimu amani kwa maendeleo ya jamii.
“Nawaombeni sana, muitunze amani yetu, kuna maisha baada ya uchaguzi, amani ikichezewa watakaopata tabu ni akina mama na watoto”, alisema Rais Magufuli.
Aidha, alisisitiza kuwa Watanzania wanahitaji kushikamana kwa pamoja na kushirikiana kwenye harakati za kujenga uchumi wa nchi na kujiletea maendeleo katika jamii na kwamba masuala ya mivutano ya kisiasa au kidini hayataifikisha nchi popote.
Katika hotuba zake Rais Magufuli amekuwa akiwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kudumisha amani kwani viongozi na waasisi wa Taifa hili wamefanya mengi yenye tija kwa taifa hili ikiwa ni pamoja na kuilinda amani tuliyonayo.
Ni ukweli usiopingika kuwa Barani Afrika tunashuhudia migogoro, vurugu za kisiasa na machafuko kwa baadhi za nchi inayosababisha kukosekana kwa amani chanzo chake kikielezwa ni kutofautiana kwa mitazamo ya itikadi za kisiasa mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Katika kampeni, Rais Magufuli amewataka wananchi kutofanya majaribio wakati wa uchaguzi akiwa na maana, Watanzania hawana budi kufikiria kabla ya kuamua kufanya maamuzi kwani watu wengi hukosea katika kufanya maamuzi hasa kwenye mambo muhimu ya maisha yao na matokeo yake ni kujilaumu.
Akihutubia wananchi wa Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, uliopo Jijini Arusha, Rais Magufuli aliwaomba wananchi kudumisha amani na kuchagua viongozi wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya wanyonge na kutatua matatizo yao kwa dhati
“Nileteeni viongozi hawa wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya wanyonge na kutatua matatizo yao kwa dhati, tunataka amani katika nchi yetu ninawaomba ndugu zangu amani tuitunze, tunahitaji amani kwa maendeleo ya taifa letu”. Alisema Rais Magufuli.
Aidha, katika kipindi hiki cha kampeni viongozi mbalimbali wa dini wamekuwa wakihubiri juu ya kuleta utulivu na amani kwa kuwa mwanadamu ameumbwa katika kisiwa cha amani chenye utulivu wa hali ya juu.
Naye, Sheikh Shaaban Juma wa Mkoa wa Arusha amesema, kazi ya viongozi wa dini ni kuhubiri amani kwa sababu amani ndio hifadhi na kinga ya kweli katika kumlinda mwanadaamu na ubinaadamu na kuliombea taifa hili lidumishe amani hata baada ya uchaguzi
“Mwanadamu hahifadhiwi kwa nyumba anahifadhiwa kwa amani, hutokana na umuhimu wa amani tunajifunza katoka katika Quraan tukufu kuwa amani ndilo jengo lenye kumhifadhi mwanadamu…..’ Alisema Sheikh Shaaban.
Naye, Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Arusha Baba Askofu Isaack Aman amesema kwa miaka zaidi ya 60 sasa Tanzania imebarikiwa kudumisha amani na umoja na kwamba katika uchanguzi utakaofanyika Oktoba 28, 2020 tupate viongozi watakaosimamia tunu za taifa letu ambazo ni amani, umoja,upendo, haki na ustawi wa kila mmoja wetu.
Wakati huo huo Baba Askofu Solomoni Masangwa wa Dayosisi ya Kaskazini Kati Kanisa la KKKT amewasihi viongozi kufanya kampeni za amani na utulivu huku akiwahimiza Watanzania kutobaguana kwa misingi ya udini na ukanda kwani huu sio wakati wa kuchagua viongozi kwa ushabiki bali kuchagua viongozi ambao wapo tayari kuleta maendeleo na kuwaunganisha Watanzania kwa pamoja.
“Hii sio saa ya kuchagua viongozi kwa ushabiki bali watu wajue tuweke viongozi walio na nia ya kuibadilisha Tanzania na kuiletea maendeleo na kuwaunganisha Watanzania kwa pamoja “ Alisema Askofu Masagwa.
Madhara ya kukosekana kwa amani na utulivu wa kisiasa husababisha matatizo mengi katika jamii ikiwezo machafuko na mapigano kati ya Serikali na vikundi vya upinzani yanayosababisha kuzuka kwa wimbi la wakimbizi. Madahara haya yanarudisha nyuma shughuli za kiuchumi na hivyo kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii kama vile afya, elimu kwa watoto na huduma za usafiri,
Matokeo mengine ya madhara haya ya machafuko ni kufunguka kwa mwanya wa uporaji wa rasilimali za taifa unaofanywa na mabereru kwa kisingizio cha kutoa misaada kwa nchi zilizokumbwa na machafuko au mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya chaguzi za viongozi wa kitaifa.
Sababu hii ndio inayofanya kiongozi yeyote mzalendo kuhubiri amani na utulivu wakati wa kampeni, kusisitiza umuhimu wa kutokufanya makosa wakati wa kufanya maamuzi kwani tumepewa muda wa kuchagua viongozi sahihi na si muda wa kufanya majaribio ya kuchagua viongozi.
Njia pekee ya kusaidia kufanya maamuzi mazuri ni kujizoeza kufikiria matokeo ya mwisho ya uamuzi tutakaofanya kabla ya kuamua, vilevile kuwa tayari kuishi na matokeo ya uamuzi huo kwa kuwa matokeo yoyote ya uamuzi tunaofanya ni matokeo ya kudumu kwa muda mrefu.
Mwisho.