OKTOBA 28, 2020 Watanzania wote waliotimiza vigezo kwa mujibu wa sheria, wanatarajia kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuwachagua Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Hatua hii muhimu imefikiwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa miezi kadhaa uliohusisha hatua za uhuishaji wa madaftari ya kudumu ya wapiga kura, uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali na kampeni.
Tume, inapenda kuchukua fursa hii kuzipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; Mosi, kwa kulipa uzito tukio hilo na kutoa fedha za kuligharamia ili wananchi waweze kutimiziwa haki yao ya kikatiba.
Pili, Tume inazipongeza Serikali zetu, kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa maandalizi mazuri na kwa mwendelezo wa utoaji elimu ya uraia kwa wananchi kuhusu uchaguzi mkuu na kwa kusimamia vyema hatua zote za mchakato wa uchaguzi kwa weledi huku zikizingatia sheria na kanuni za nchi, haki, usawa, usalama na amani.
Pia Tume inalipongeza Jeshi la Polisi kwa kulinda usalama wa raia na mali zao katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi. Vilevile, Tume inavipongeza vyombo vya habari kwa kuzingatia haki ya kikatiba ya wananchi kwa kuwahabarisha kuhusu matukio na sera zilizokuwa zinanadiwa na wagombea na vyama vyao na elimu iliyokuwa ikitolewa na wadau mbalimbali katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi. Jambo hilo limetoa fursa kwa wananchi kuwasikiliza na kuwapima wagombea wa vyama mbalimbali na litawasaidia kuchagua viongozi sahihi siku ya upigaji kura.
Mwisho, Tume inawaasa wananchi wote raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kutimiza wajibu wao wa kuzingatia sheria na kanuni za nchi kwa kuhifadhi amani katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
Katika kipindi hiki cha siku tatu zilizobakia kuhitimisha mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2020, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapenda kutoa wito ufuatao kwa wadau mbalimbali:
- Wananchi
Wajitokeze kwa wingi na kutumia vyema haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi watakaodumisha amani, umoja na mshikamano nchini na kuliletea maendeleo Taifa letu.
- Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama
- Wasimamie amani ili watanzania waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura katika hali ya utulivu na amani na kuchagua viongozi bora.
- Wanapotekeleza majukumu yao wazingatie maadili, waheshimu haki za binadamu na na mising i ya utawala bora na waepuke matumizi makubwa ya nguvu yasiyokuwa ya lazima.
3. Mamlaka zenye dhamana ya kusimamia uchaguzi
- Zihakikishe uchaguzi mkuu unasimamiwa kwa haki na amani wakati wote.
- Wadumishe amani wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa wazi, wenye amani na utulivu.
- Viongozi wa dini
Waendelee kukemea maovu na kuliombea taifa katika kipindi hiki muhimu ili haki, amani, utulivu na upendo viendelee kudumishwa sasa na hata baada ya uchaguzi kumalizika.
- Wagombea watakaoshindwa
Kwa kuwa katika kila ushindani ni lazima awepo mshindi na atakaeshindwa, wagombea watakaoshindwa wanaombwa wakubali matokeo ili kudumisha amani ya nchi yetu. Ambaye hataridhishwa na matokeo, ni vema akafuata mkondo wa sheria na kanuni zilizowekwa zinazoruhusu kudai haki badala ya kutafuta njia za mkato katika kudai haki ambazo matokeo yake yanaweza kuwa hasi.
Tume inawatakia Watanzania wote Uchaguzi mwema
Mungu ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!