Mwenyekiti wa kijiji cha Makande kata ya Lukumbule wilayani Tunduru Silaju Said aliyenyoosha mkono katikati akiwaonesha baadhi ya wataalam wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Afisa kilimo anayeshughulikia mazao Gallus Makwisa wa kwanza kulia,afisa ushirika George Bisan wa pili kushoto na mjumbe wa chama kikuu cha ushirika Tamcu Ltd Zainabu Yassin.
Baadhi ya wananchi viongozi wa Serikali ya kijiji cha Makande na wataalam wa kilimo ba ushirika kutoka halmashauri ya wilaya Tunduru wakikagua eneo la shamba lililopangwa kutumika kwa ajili ya mradi wa kilimo cha ufuta katika msimu wa 2020/2021.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
SERIKALI ya kijiji cha Makande kata ya Lukumbule wilayani Tunduru kilichopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Msumbuji,kimetoa ardhi yenye ukubwa wa ekari 3,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa kilimo cha zao la ufuta katika msimu wa 2021.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Silaju Said alisema, hapo awali eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya makazi ya jeshi la wananchi Tanzania, hata hivyo serikali ya wilaya ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro wameona ni vizuri eneo hilo liwe sehemu ya mradi wa kilimo cha ufuta kutokana na ardhi yake kuwa mzuri kwa kilimo.
Alisema, katika mradi huo makundi mbalimbali ikiwemo shule, muungano wa vyama vya wakulima(Mviwata) yatapewa maeneo ambapo ameipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuimarisha zao la ufuta ambalo ni la pili kuwaingizia fedha nyingi wakulima wa wilaya ya Tunduru .
Alisema, wametoa eneo hilo kwa manufaa ya jamii na pia itasaidia wakazi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani kwenda kujifunza kilimo bora cha ufuta pindi mradi utakapoanza na utafungua fursa kwa wakulima kupata masoko na taasisi mbalimbali kwenda kuwekeza katika shamba hilo.
Baadhi ya wananchi wa Makande Adinan Kihosa na Tabia Ali wameshukuru kupelekewa mradi wa kilimo cha ufuta kwani mbali kuwapatia kipato cha uhakika,pia utasaidia kupata elimu ya kilimo cha kisasa ambacho kitakwenda kumaliza suala la umaskini wa kipato katika familia zao.
Tabia Ali alisema, mbali ya mradi huo kuwa sehemu ya kujifunza kama shamba darasa utakwenda kupunguza tatizo la vijana wengi kukaa vijiweni, kwa sababu baadhi yao watapata shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato.
Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia Benki ya maendeleo ya kilimo ambayo ndiyo itatoa fedha za mradi kuhakikisha inatoa fedha hizo mapema ili wakulima na vikundi vitakavyoingizwa kenye mradi huo waweze kuwahi msimu wa kilimo kwani tayari mvua za kwanza zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tunduru.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa wilaya ya Tunduru Gallus Makwisa alisema,mradi wa kilimo cha ufuta katika wilaya hiyo umelenga sana vikundi vidogo vidogo ambavyo vitaungana pamoja na vitapata fedha kutoka kwa chama kikuu cha ushirika TAMCU ambayo imebeba dhamana ya kusimamia mradi huo.
Alisema, mradi wa kilimo cha ufuta umegawanyika katika meneo mawili ambayo ni shamba la ushirika kijiji cha Pacha nne kata ya Namiungo ambalo litachukua vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na pili ni shamba la Makande ambalo litahusisha kwa vikundi maalum vilivyoonesha nia ya kulima zao hilo.
Kwa mujibu wake, kwa kuanzia mradi huu utaanza kwa kilimo cha kutegemea mvua ambapo hunyesha kuanzia katikati ya mwezi Novemba,hivyo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba inatakiwa mashamba yote yawe yamelimwa ili mwishoni mwa mwezi Desemba kazi za kupanda zianze na kukamilika katikati ya mwezi Januari kwa kuwa maeneo hayo yamezungukwa na maji.
Alitaja mategemeo ya mradi ni kuleta tija kwa wana vikundi kujitegemea kiuchumi kutokana na faida itakayopatikana kwenye mradi na kuacha kutegemea chanzo kimoja cha mapato ambacho ni ushuru wa mazao,kuongezeka uzalishaji wa ufuta,kutoa ajira kwa baadhi ya wana vikundi ambapo zaidi ya watu 20,000 hususani vijana watapata ajira.
Alisema, kwa kuanzia chama kikuu cha Ushirika Tamcu ambacho ndiyo wasimamizi wakuu wa mradi huo kimejipanga kuomba kwa makubaliano maalum taasisi ya Magereza na vijana wa jeshi la akiba kufanya kazi katika mashamba yote mawili.