Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Stella Ikupa, akifungua mafunzo ya Usalama na Afya kazini kwa makundi mbali mbali ya watu wenye ulemavu. Aliyeambatana nae ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda. Mafunzo hayo yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akizungumza na washiriki wa mafunzo ya Usalama na Afya kazini kwa watu wenye ulemavu wilayani Rufiji (hawapo pichani) alipoambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Stella Ikupa, ambaye alikwenda kufungua mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya kuongeza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi wakiwafuatilia wakufunzi wa mafunzo hayo (hawako pichani). Mafunzo hayo yaliandaliwa na OSHA na kutolewa kwa watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na kilimo pamoja na ufundi mbali mbali katika Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
*********************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali imewahakikishia watu wenye ulemavu kwamba itaendelea kuwawezesha kwa namna mbali mbali ikiwemo kuwapatia elimu ya Usalama na Afya kazini ili wawaze kutoa mchango wao kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Stella Ikupa, wakati akifungua mafunzo ya Usalama na Afya yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa watu wenye ulemavu Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
Ikupa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii hivyo itaendelea kuliwezesha kundi hilo kwa kuweka mazingira rafiki ya uzalishaji kupitia Taasisi zake ikiwemo OSHA.
“Serikali kupitia Taasisi kama OSHA na nyinginezo na kwakushirikiana na wadau mbali mbali kama vile Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA); tutaendelea kuwapa mafunzo mbali mbali yakiwemo mafunzo kuhusu masuala ya Usalama na Afya kazini.
Aidha, tutaendelea kuwawezesha kiuchumi kwa kuwatafutia masoko ya mazao na bidhaa mnazozalisha na kuhakikisha kwamba kunakuwepo na fursa za uwezeshaji ikiwemo upatikanaji wa mitaji,” alisema Naibu Waziri.
Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo, Kiongozi huyo wa Wazara anayeshughulikia Masuala ya Watu wenye Ulemavu, aliwaagiza OSHA kuendelea kutoa mafunzo ya kujilinda dhidi ya vihatarishi vya kiusalama na afya katika sehemu za kazi kwa makundi mbali mbali ya watu wenye ulemavu kote nchini ili kuwawezesha kufanya kazi katika hali ya afya njema na usalama unaostahili.
Aidha, Waziri Ikupa aliwakumbusha washiriki wa mafunzo husika kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 kushiriki kuwachagua viongozi wao katika ngazi mbali mbali ambao watawaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Taasisi yake wa kuyafikia makundi mbali mbali katika jamii na kutoa mafunzo ya Usalama na Afya yatakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni za afya na usalama.
“Hii sio mara ya kwanza kwa Taasisi yetu kutoa mafunzo kama haya kwa watu wenye ulemavu. Tumeshafanya mafunzo hayo katika mikoa mingine ikiwemo Kagera na Dar es Salaam na kwakuwa ni sehemu ya mkakati wa OSHA basi niwahakikishie kwamba mafunzo haya yatendelea kutolewa katika maeneo mbali mbali ya nchi kwa makundi mbali mbali ya watu,” alieleza Khadija Mwenda ambaye ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo Walusimbi Abdul na Zuberi Abukari wameipongeza OSHA kwa kuwapa mafunzo na kutoa wito kwa Mamlaka hiyo kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa makundi mbali mbali wakiwemo watu wenye ulemavu kwa nchi nzima.
OSHA ni Mamlaka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) ambayo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
Miongoni mwa majukumu ya Taasisi hii ni kuongeza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya kazini kwa wadau na wananchi wote kwa ujumla wakiwemo watu wenye ulemavu.