RS Berkane wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Pyramids kwenye mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Prince Moulay Abdallah Jijini Rabat, Morocco.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Mohssine Iajour dakika ya 15 tu ya mchezo huo, akiiwezesha RS Berkane kuiangusha timu ya Misri, Pyramids na kutwaa taji lao la kwanza kabisa la Kombe la Shirikisho wakicheza fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.
Mwaka jana, timu hiyo ya Morocco ilifungwa kwenye fainali na timu nyingine ya Misri, Zamalek SC, lakini hawakuwa tayari kuendeleza uteja kwa majirani zao hao wa Kaskazini mwa Afrika, tena kwenye ardhi yao wenyewe, Rabat.
Michuano hiyo imechelewa kumalizika mwaka huu kutokana na kusimama tangu katikati ya Machi ikiwa katika hatua ya Nusu Fainali kwa sababu ya mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona, vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likaagiza Nusu Fainali zisogezwe mbele hadi Oktoba 2020 katika kituo kimoja, Morocco na kwa mara ya kwanza fainali ya michuano hiyo imefanyika Uwanja mmoja, Prince Moulay Abdellah, Rabat, Morocco.