Wawakilishi kutoka umoja qa Ulaya, mashirika ya kupambana na uharibifu wa mazingira na waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja.
Waandishi wa habari wakifutilia majadiliano kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
…………………………………………………………
NA SULEIMAN MSUYA
UMOJA wa Ulaya (EU) na Bara la Afrika zinahitaji kuchagua mustakabali usioongeza hewa ukaa, matumizi bora ya rasilimali na wenye kuweza kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Hayo yamesemwa na Jutta Urpilainen
Kamishna wa Ulaya wa Ushirikiano wa Kimataifa katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya Mabadiliko ya Tabianchi duniani yaliyofanyika Novemba 23/2020.
Urpilainen alisema mafanikio yao yatategemea kuungana na nchi mbalimbali wanazoshirikiana nazo kupitia ushirikiano wa kimataifa, pamoja na makubaliano ya biashara na mipango ya kimazingira. “Kwa hili, tunahitaji washirika na ushirikiano,” alisema .
Alisema ushirikiano muhimu ni ule walionao na jirani zao wa karibu, bara pacha na mshirika wa miaka mingi ambaye ni Afrika.
“Tunaweza kufanikisha hilo kwa kuwa na ushirikiano thabiti wa kimataifa wenye malengo makubwa. Hii inamaanisha kupendekeza hatua jumuishi zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, na kuzingatia masuala ya kiuchumi na kijamii.
Tunapaswa kuweka mkazo juu ya kuwa na maendeleo ya haraka katika maeneo yafuatayo yenye uwezo wa kuwa na faida kubwa kwa mabara yetu mawili: nishati endelevu na mifumo ya chakula, kulinda bioanuwai kwa kurejesha mifumo ya ikolojia, kupambana, usafirishaji haramu wa nyara za wanyamapori, usimamizi endelevu wa misitu, ardhi na maeneo ya hifadhi.
Kwa mfano, katika mradi wetu wa Eco-Boma nchini Tanzania, tumejenga mfumo wa kukabiliana na tabianchi kwa wafugaji wa jamii ya Kimasai kwa kuboresha upatakinaji wa maji kwa ajili ya mifugo, usimamizi wa nyanda za malisho, huduma za afya za mifugo, kilimo kinachostahimili ukame, nishati na elimu ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema Kamishna.
Kamishna Urpilainen alisema jambo moja la uhakika ni kwamba mabadiliko ya kimazingira yatahitaji uwekezaji mkubwa ambapo fedha za umma pekee hazitatosha.
“Hii ndio sababu ambayo tunashughulikia kupunguza athari za uwekezaji ili kuwezesha ushiriki mkubwa zaidi wa sekta binafsi barani Afrika na kuunga mkono maendeleo yanayozingatia mazingira kwa wote,” alisisitiza.
Alisema wakati dunia inapambana na janga la afya, na athari zake, ushirikiano wa kimazingira kati ya Afrika na Ulaya utakuwa muhimu katika miaka ijayo.
Aliongeza kuwa EU itashirikiana na Tanzania na kuunga mkono juhudi zake katika kuleta maendeleo yanayozingatia mazingira ambayo huhakikisha uchumi unakuwa na mustakabali imara na wenye faida kwa wote.
“Kufanya kazi pamoja kwa maslahi yetu ya pamoja, Afrika na Ulaya zinaweza “kujenga tena kwa ubora kwa kujenga dunia kijani, endelevu na jumuisha zaidi kwa wote,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miezi michache iliypopita, dunia yetu imebadilika kwa namna ambayo hatungeweza kutegemea mwaka mmoja uliopita.
Kamishna alisema, hata kabla ya janga la COVID-19 kuikumba dunia, dunia ilikukuwa imeshaanza kuyumba katika mwendeleo wao kuelekea katika mustakabali endelevu.
Urpilainen alisema walikuwa tayari wanakabiliwa na matatizo yanayohusiana na tabianchi, upotezaji wa bioanuwai na uchafuzi wa mazingira.
Alisema kulihitajika hatua kuchukuliwa ili kurudisha mwelewano kati ya dunia na uchumi, na Umoja wa Ulaya ukachukua hatua muhimu katika hilo kwa kuzindua Mpango wa Kijani wa Ulaya.
“Kuanzia namna ambavyo tunazalisha bidhaa zetu hadi tunavyozitumia, Mpango wa Kijani ni mkakati wa ukuaji wenye malengo makubwa ambao unakusudia kupambana na changamoto kubwa za tabianchi na mazingira ambazo zinatukabili,” alisema.