Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo
akikabidhi usafiri wa Baiskeli na Vipaza sauti kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya
Jamii wilayani hapo juzi kama nyenzo muhimu zitakazowasaidia. kurahisisha
utekelezaji wa majukumu yao.
Lishe na Mratibu wa Huduma za Jamii wilayani hapo, Agnes John akisoma taarifa
fupi ya Mradi wa Boresha Lishe kwenye Halmashauri ya Ikungi.
wa Baiskeli hizo.
Mkuu wa Wilaya Mpogolo akiendesha hafla hiyo.
Tawala wa Wilaya ya Ikungi (DAS), Winfrida Funto (katikati) akifuatilia kwa
makini makabidhiano hayo, kulia ni Afisa Tarafa, Josephine Kadaso na DC
Mpogolo.
Mradi wa Boresha Lishe kutoka shirika la SEMA, Hudson Kazonte akizungumzia tija
ya mradi huo na namna usafiri huo wa baiskeli utakavyopunguza changamoto ya
utoaji huduma.
Na Godwin Myovela, Ikungi
SERIKALI kwa kushirikina na Umoja wa Nchi za Ulaya na Shirika
la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imetoa jumla ya baiskeli 103 kwa wahudumu
wote wa afya ngazi ya jamii sambamba na ‘vipaza sauti’ vyenye idadi kama hiyo
wilayani hapa, lengo ni kuwapunguzia changamoto ya usafiri wakati wakitekeleza
majukumu yao.
Katika kuboresha afya ya uzazi na lishe, kupitia mradi wa
‘Boresha Lishe’ serikali kupitia halmashauri ya Ikungi kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali, wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ya ‘SEMA’ na ‘RECODA’
imeazimia kupunguza udumavu wa siku 1000 za mtoto-yaani tangu kutungwa kwa
mimba hadi anapofikisha miaka 2.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi baiskeli hizo ofisini
kwake jana, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo aliwataka waliokabidhiwa
baiskeli hizo kuhakikisha wanazitunza na zinatumika kwa malengo kusudiwa.
“Niwasihi muwe waangalifu na mzitunze baiskeli hizi,
serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwenye sekta ya afya hususani
kwenye eneo hili la afya ya uzazi na lishe, azma ikiwa ni kuhakikisha tunaondoa
kabisa kiwango cha utapiamlo wa udumavu kutoka asilimia 7 mpaka 0,” alisema
Mpogolo.
Aidha, aliyashukuru mashirika na nchi wahisani wanaoendelea
kushirikiana na serikali katika kutekeleza mradi wa Boresha Lishe kwa vijiji 43
kuzunguka Ikungi huku akisisitiza ni mradi wenye tija kwa makundi yote ya jamii
wilayani hapo, na hasa akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya
miaka miwili.
Naye Afisa Lishe na Mratibu wa Huduma za Jamii wilayani
hapo, Agnes John, alisema Halmashauri ya Ikungi ina jumla ya Kata 28 na Vijiji
101 vyote vina wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii, na wote wamepatiwa mafunzo ya
msingi ya awali ya afya ya uzazi na lishe.
Halmashauri ya Ikungi ina jumla ya wakazi 329,520, ambapo
watoto chini ya miaka mitano ni 58,707, na wanawake wenye umri wa kuzaa (miaka
15-49) wanafikia 22,884.
“Mafanikio tuliyoyapata mpaka sasa ni kujikwamua mapema
kwenye rangi nyekundu, kwa miaka miwili mfululizo mpaka sasa viashiria vyote
vinavyohusiana na huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii vina alama ya
kijani kuashiria tunafanya vizuri,” alisema John.
Aidha, mratibu huyo alisema hata kiwango cha utapiamlo wa
udumavu kimepungua kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 5, wakati kimkoa ni
asilimia 29.8. Alisema ukondefu umepungua kutoka asilimia 1 hadi kufikia 0.4,
wakati kimkoa ni asilimia 4.7.