**********************************************
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli amemtuma aje amuombee kura kwenye mikoa ya Kusini na amesema hatowaangusha.
“Mheshimiwa Rais amenituma nije kumuombea kura kwa sababu wakati anapanga kuja huku kama ilivyokuwa kwenye ratiba ya Tume ya Uchaguzi, akapata ugeni wa kitaifa kutoka kwa Rais wa Malawi, Mheshimiwa Dkt. Lazarus Chakwera.”
“Malawi ni jirani zetu, asingeweza kuwaacha. Tume ikishakupangia ratiba na ikapita na wewe hukwenda, haisogezwi mbele bali wanaangalia kama huko mbele utakuwa na nafasi wanakupangia tena,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Likongowele, wilayani Liwale, mkoani Lindi kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Ujenzi wilayani humo.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko Lindi kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwanadi mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na madiwani 20 wa kata za jimbo hilo.
Amewaomba wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli kwa sababu urais unataka mtu makini atakayejali mahitaji ya watu wanyonge na mwenye mawazo ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
“Lazima tumpate Rais anayeguswa na mahitaji ya wanyonge, anayeweza kusimamia huduma za jamii ili ziwafikie wananchi wote, na mtu huyo si mwingine bali ni Dkt. Magufuli. Jumatano ya keshokutwa, nenda kapige kura kwa Dkt. Magufuli, hata kama unatoka upinzani, kampigie Dkt. Magufuli ili atuletee maendeleo,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakazi wa Liwale na wa mkoa mzima wa Lindi wamshukuru Rais Magufuli kwa mambo mazuri aliyowafanyia. “Lazima tumshukuru kwa yote aliyotufanyia kwenye mkoa wetu na Watanzania kwa ujumla kwa kumpa kura nyingi za kishindo,” amesisitiza.
“Ni lazima tumshukuru kwa kuniteua niwe msaidizi wake wa karibu. Kwani kuna mikoa mingapi hadi auchague mkoa huu? Kuna Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 200 ndani ya Bunge, lakini aliomuona mtoto wenu anafaa na ndipo akamchagua awe msaidizi wake wa karibu,” amesema.