Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akimkabidhi baadhi ya vifaa tiba vya macho kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Dkt. Hashim Mvogogo wakati wa uzinduzi wa jengo la wagonjwa wa macho wa nje mjini Sumbawanga.
Baadhi ya wananchi wakiwa wamekaa nje ya jengo la Wagonjwa wa macho wa nje kabla ya kuzinduliwa kwake.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akisalimiana na Mha. Baba Askofu Beatus Urassa wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga muda mfufi baada ya kuzindua jengo la wagonjwa wa macho wa nje. Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (waliokaa katikati) Mha. Baba Askofu Beatus Urassa wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga (wa pili toka kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (wa pili toka kulia) Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu (wa kwanza kulia) pamoja na mwakilishi wa Shirika la Ujerumani DKVB Dkt. Karsten Paul (wa kwanza kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na watumishi na wataalamu mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa jengo la wagonjwa wa nje wa macho katika hospitali ya kumbukumbu ya Dkt. Atman Sumbawanga.
***************************************
Katika kusaidia juhudi za serikali kuboresha huduma katika mkoa wa Rukwa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga kwa ufadhili wa Shirika la German Committee for Prevention of Blindness (DKVB) limezindua jengo la wagonjwa wa nje wa macho katika hospitali teule ya Kumbukumbu ya Dkt. Atman mjini Sumbawanga ili kusogeza huduma kwa wagonjwa wa macho ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu nje ya mkoa kufuata huduma hiyo.
Wakati akitoa taarifa fupi ya program ya macho kwa mikoa ya magharibi mwa Tanzania (Rukwa, Katavi na Kigoma) Msimamizi wa Mradi huo Ryner Linuma alisema kuwa tangu Novemba, 2017 shirika hilo lilipoanza kutoa huduma zake katika mkoa wa Rukwa kwa njia ya mkoba (Eye Care Surgical Outreach Camp) hadi Oktoba, 2019 jumla ya watu 4,296 walikuwa wamepatiwa huduma, ambapo 977 ka ti ya hao walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, 526 walipatiwa miwani, 22 walipatiwa rufaa kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili na KCMC.
“Baada ya kuona idadi ya wahitaji wa huduma za macho kuwa kubwa na kuongezeka karibu kila kambi ya huduma ya macho inapofanyika, shirika liliona kuwa majuma mawili ya kambi hayatoshi na mfumo huu wa huduma za macho kwa mfumo wa Mkoba sio endelevu katika meneo haya, hivyo likaanza kufikiria namna ya kufanya huduma hizi kuwa endelevu ndipo shirika liliposhirikisha serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga mwezi April,2019 na kufanya kikao,”
“Baada ya kikao hicho ikaanzishwa program maalum ya kuzuia upofu unaoweza kuzuilika katika mikoa ya magharibi mwa Tanzania kupitia utoaji wa huduma jumuishi za macho ikiwa na malengo ya kusomesha wataalamu waajiriwa wa Serikali na Jimbo Katoliki katika ubobezi wa utoaji wa huduma za macho, Kujenga jingo maalum la huduma za macho na vifaa tiba na kuendeleza mahusiano baina ya sekta binafsi na umma katika kutoa huduma endelevu za macho ndani ya Mkoa,” Alielezea.
Kwa upande wake mgeni rasmi wa tukio hilo Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo alisema kuwa anatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga kusaidia juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya katika mkoa ambapo kati ya vituo 239 vya kutolea huduma za afya ndani ya mkoa, vituo 21 vinamilikiwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga na kuongeza kuwa Hospitali ya Kumbukumbu ya Dkt. Atman ya Sumbawanga Mjini na Hospitali ya Namanyere Wilayani Nkasi zimekuwa zikitumika kama hospitali teule za halmashauri.
“Kabla ya kuhitimisha naomba nirudie tena kuwashukuru wadau wetu kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia kama serikali kupitia watumishi, vifaa na sasa jingo hili lenye thamani ya shilingi 343,888,580/=. Niwaombe wadau mnaohusika katika usimamizi wa huduma hizi kuhakikisha watumishi wote waliopatiwa mafunzo kupitia ufadhili huu wanatumika ipasavyo kuboresha huduma za macho katika mkoa kupitia kituo hiki na vituo vingine vilivyotajwa,” Alisisitiza.
Aidha Wakati akitoa neno la shukurani Mha. Baba Askofu Beatus Urassa wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga aliwashukuru wafadhili pamoja na ushirkiano uliooneshwa na serikali katika kuhakikisha ujenzi wa jingo hilo unakamilika na wananchi wa Mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani wanapata huduma ambayo haijawahi kupatikana hapo awali.
“Kwa kadiri ninavyoufahamu mpango kazi wa Shirika hili la German Committee for Prevention of Blindness, makabidhiano haya na uzinduzi wa jengo hili la wagonjwa wa macho wa nje ni ngazi ya kuelekea mradi mkubwa Zaidi wa ujenzi wa Chumba cha upasuaji wa macho kuanzia muda wowote kabla ya mwaka 2021 na kutoa vifaa tiba pamoja na usafiri kwaajili ya program hii ya huduma za macho,”
Halikadhalika, Mwakilishi wa Shirika la German Committee for Prevention of Blindness Dkt. Karsten Paust aliishukuru serikali kwa ushirikiano uliopo katika kukamilisha azma hiyo ya kutoa huduma bora ya macho kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na mikoa ya magharibi mwa Tanzania.
Miongoni mwa mafanikio ya programu hiyo ni pamoja na kuwasomesha na kuwapatia vifaa tiba wauguzi 22 katika fani ya macho kutoka halmashauri nne za mkoa huo, kumsomesha mtaalamu mmoja wa miwani, kumsomesha daktari bingwa wa macho mmoja, kuwasomesha madaktari watatu wa upasuaji wa mtoto wa jichona kuanzisha mradi wa elimu ya afya ya macho katika halmashauri zote za mkoa.