………………………………………………………………………
NA MWANDISHI WETU
WAPENZI wa muziki, hasa wa dansi na burudani kwa ujumla, wikiendi hii inatarajiwa kuwa ya aina yao kwao pale watakaposhuhudia shoo kali na ya kijanja itakayoporomoshwa na mkali wa dansi nchini, Christian Bella kwenye Hoteli ya Dynasty Beach Resort iliyopo Ununio, jijini Dar es Salaam.
Bella, maarufu kama King of Melodies , hatakuwa peke yake, bali ataambatana na bendi yake ya Malaika, lakini pia kijana aliyeibuliwa na Bongo Star Search (BSS), Kayumba, naye atakuwapo siku hiyo kufanya vitu vyake.
Usiku huo uliopewa jina la Full Moon Party, unatarajiwa kuwa wa aina yake kwani mbali ya burudani ya muziki kutoka kwa Bella na bendi yake hiyo pamoja na Kayumba, pia kutakuwa na mambo lukuki yatakayoifanya siku hiyo kuwa ya kukumbukwa.
Warembo wanaoshiriki shindano la Miss Utalii Tanzania 2020, nao watakuwapo katika tukio hilo kunogesha usiku huo wa aina yake.
Akizungumzia shoo hiyo itakayofanyika Jumamosi, Bella aliahidi kufanya makamuzi ya aina yake akishirikiana na bendi yake ya Malaika, akiwataka wapenzi wa burudani kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
“Tukutane Jumamosi ya Oktoba 31 kwenye Full Moon Party itakayofanyika Dynasty Beach Resort, usikose, nitafanya shoo ‘live’ nikiwa na timu nzima ya Malaika Bendi, tutagonga ngoma zote kali ‘live’, muziki bomba burudani kali ndani ya Dar es Salaam.
“Usikose kabisa ndani ya Full Moon Party, itatisha hatari sana, njoo na rafiki, njoo na mtu ambaye unamkubali, mtu ambaye unampenda, njoo naye Dynasty Beach Resort upate burudani kali na upepo mwanana wa Bahari ya Hindi. Kuna vyakula vya kila aina vya ubora wa hali ya juu na vinywaji kede kede kwa bei ya kawaida sana,” alisema Bella.
Alisema kwa upande wake na wanamuziki wa Bendi ya Malaika, wamefanya maandalizi ya hali ya juu ili kutoa burudani ya kiwango cha kimataifa itakayokonga nyoyo za wote watakaofika Dynasty Beach Resort siku hiyo.
Alisema kama ilivyo kawaida yao, anaamini kila atakayefika Dynasty Beach Resort, hatajuta kupoteza muda wake kwa burudani kali watakayoitoa usiku huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dynasty Beach Resort, Manase Mwakale, amesema kuwa maandalizi yote juu ya usiku huo wa Full Moon Party, yamekamilika.
Aliwataka wapenzi wa burudani wa Dar es Salaam na vitongoji vyake, yakiwamo maeneo ya Mkoa wa Pwani, Morogoro na hata Tanga, kujitokeza kwa wingi usiku huo kwani kuna mambo mengi mazuri wamewaandalia.
“Tunawakaribisha sana wapenzi wa burudani wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani katika usiku wa Full Moon Party utakaofanyika Hoteli ya Dynasty Beach Resort yenye hadhi ya kimataifa.
“Siku hiyo kutakuwa na matukio mengi tu ya burudani, ikiwamo bendi ya Malaika chini ya kiongozi wake, Christian Bella ambao watatoa burudani ya aina yake. Pia, atakuwapo msanii wa muziki wa kizazi kipya, Kayumba pamoja na warembo wanaoshiriki mashindano ya Miss Utalii Tanzania 2020,” alisema.
Mbali ya vyakula, vinywaji na huduma bora vinavyopatikana Dynasty Beach Resort, Mwakale alisema kuwa pia kutakuwa na ‘screen’ kuonyesha mechi za ligi mbalimbali za Ulaya, hivyo wapenzi wa soka wanaweza ‘kuua ndege wawili kwa jiwe moja’.
Alisema kuwa burudani itaanza mapema tu na kumalizika alfajiri, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kwenye maeneo yote ya hoteli yao hiyo.
Alisema kuwa tiketi za viingilio vya shoo hiyo iliyodhaminiwa na Windhoek Lager ni shilingi 10,000 kwa kawaida, shilingi 20,000 premium na shilingi 30,000 kwa upande wa VIP.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Dynasty, tiketi za Full Moon Pary, zimeshaanza kuuzwa kwenye vituo mbalimbali, ikiwamo mgahawa wa Royal Oven ya Victoria, Mikocheni na Mbezi pamoja na Engen Petrol Station Makonde Mbezi Beach, Mawela Store na Dynasty Beach Resort.