Na Dotto Mwaibale
WANANCHI nchini wametakiwa kuilinda amani siku ya kupiga kura na kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
Ombi hilo linetolewa jana na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila wakati wa maombi maalumu ya kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, 2020.
Akihubiri katika maombi hayo Ndabila alisema wameamua kufanya maombi hayo kwa sababu mara nyingi unapofanyika uchaguzi kunakuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuashiria uvunjivu wa amani na utulivu wa nchi yetu.
Alisema kufuatia kuwepo kwa changamoto hizo ambazo amekuwa akiziona zikifanyika katika nchi kadhaa wanafanya maombi hayo ikiwa ni kukumbushana kuitunza amani katika kipindi hiki kwani baada ya uchaguzi maisha yataendelea.
“Kanisa lina hekima ya kuvielekeza vyama vya siasa kwa njia ya maombi ili viwe na busara ya kufanya uchaguzi bila ya kuharibu amani na utulivu wa nchi uliopo.” alisema Ndabila.
Ndabila aliwapongeza wagombea wa vyama vya siasa kwa kuonesha kuilinda amani ya nchi katika kipindi chote cha kampeni licha ya kuwepo changamoto ndogo ndogo na akaviomba vyama hivyo viendelee kufanya hivyo hata siku ya kupiga kura.
Alisema jambo linalo mpa amani ya kupiga kura kwa amani siku hiyo ni kila mgombea anapokuwa kwenye kampeni kuanza mkutano wake kwa kumtanguliza Mungu.
Ndabila alisema amani inapokosekana wa kulaumiwa ni viongozi wa dini kwa sababu ndiyo wenye wajibu wa kuhamasisha waumini wao kumuomba Mungu atuepushe na uvunjifu wa amani wakati wote na hasa inapofika kipindi cha uchaguzi.
“Wagombea wote ni watoto wa Mungu hivyo wanapaswa kumtii Mungu ili wasilete machafuko katika nchi yetu,” alisema Ndabila.
“Nimesikiliza kwa makini sera za wagombea mbalimbali wote wana kiu ya kuona mabadiliko ya kiuchumi, kiafya na kijamii ni vema sana! napenda kuwakumbusha mabadiliko yalipohitajika yaani ya kujitawala wenyewe Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alitumia hekima na kumtanguliza Mungu na kwa hekima zake tukawa mojawapo ya nchi iliyopata Uhuru bila kupoteza maisha ya watu wake” aliongeza Ndabila.
Ndabila aliomba hekima iongoze Tume ya Taifa ya Uchaguzi itende haki, hekima iviongeze vyama vya siasa, hekima iviongoze vyombo vya usalamau na tuazimie kuto watoa watanzania kafara na kupoteza maisha ya mtanzania hata mmoja.
Aidha Askofu Ndabila alisema tusijiharibie CV kwa kuchochea machafuko kibiblia penye machafuko yoyote yale Mungu hayupo haijalishi mwenye kuyasababisha ni nani? kwani hakuna kitu ambacho Mungu anakichukia kama kuharibu nchi ambayo kimsingi alituma tuitunze na imeandikwa katika zaburi ya 119:119 tukifanya ubaya katika nchi yetu kuna kuondolewa bila heshima yeyote.
Ndabila alitumia maombi hayo kuwaombea kwa Mungu Marais wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu , Masipika pamoja na mke wa Rais Mama Janeth Magufuli Mungu awape busara na hekima za kumshauri Rais wetu ili aweze kuivusha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Katibu wa kanisa hilo, Jane Magigita aliwahimiza waumini wa kanisa hilo na wananchi waliokuwepo kwenye maombi hayo kujitokeza kwenda kupiga kura ya kumchagua Rais, wabunge pamoja na madiwani na akawaomba watanzania kuombea uchaguzi huo ili Mungu atujalie kuwapata viongozi watakaoliongoza vema Taifa letu la Tanzania.
“Viongozi wa dini ni watu muhimu kwani wananguvu ya kupeleka ujumbe haraka kwa waumini wao kupitia mahubiri yao hivyo niwaombe katika hizi siku mbili zilizosalia wahamasishe kulinda amani ya nchi na waumini wao wenye sifa ya kupiga kura wajitokeze na kadi zao za kupigia kura katika vituo walivyo jiandikisha ili kutimiza haki yao ya msingi na ya kikatiba.” alisema Magigita.
Aidha Magigita alisisitiza umuhimi wa kila mtanzania kuzingatia misingi ya amani na utulivu wakati mchakato huo wa upigaji kura ukiendelea, ikiwemo kufika mapema kituoni kupiga kura na kuondoka kuelekea kwenye majukumu mengine kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kuepusha madhara au viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza.