Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Dodoma, Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa jinsi walivyoweza kurejesha fedha kwa wananchi wawili wanyonge walizokuwa wamedhulumiwa jijini Dodoma.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Dodoma, Sosthenes Kibwengo,akimkabidhi Mwalimu Mstaafu Bw.Stanley Matonya,Mkulima wa kijiji cha Itiso wilaya ya Chamwino,kiasi cha sh. Milioni 22.4 alizokuwa amedhulumiwa na Kampuni ya ya Kabugama (Kabugama Co.LTD) ya jijini Dodoma tangu mwaka 2016.
Mwalimu Mstaafu Bw.Stanley Matonya,Mkulima wa kijiji cha Itiso wilaya ya Chamwino akiwa na Mke wake wakionyesha kiasi cha sh.Milioni 22.4 kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) alizokuwa amedhulumiwa na Kampuni ya Kabugama (Kabugama Co.LTD) ya jijini Dodoma tangu mwaka 2016,Kwa kusaidiwa na TAKUKURU Mkoa wa Dodoma walivyoweza kumsaidia kurejeshewa fedha zake.
Mwalimu Mstaafu Bw.Stanley Matonya,Mkulima wa kijiji cha Itiso wilaya ya Chamwino akitoa neno la shukrani kwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma baada ya kumsaidia kurejeshwa kwa kiasi cha sh.Milioni 22.4 alizokuwa amedhulumiwa na Kampuni ya Kabugama (Kabugama Co.LTD) ya jijini Dodoma tangu mwaka 2016.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Dodoma, Sosthenes Kibwengo,akimkabidhi Bw.Ahmed Talibu,Mkazi wa Jijini Dodoma ambaye ni Mzazi wa Mtoto Nasra Ahmed Talib kiasi cha Sh.Milioni 6.49 zikiwa ni malipo ya fidia ya Kiwanja namba 214 Kitalu G Kikuyu South Extension Dodoma kilichotwaliwa kwa ajili ya kupisha Mradi wa ujenzi wa Reli ya Mwendokasi.
Mkazi wa jijini Dodoma ambaye ni Mzazi wa mtoto Nasra Ahmed Tali Bw.Ahmed Talibu,akitoa pongezi kwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma kwa kumsaidia kupatikana kwa fedha kiasi cha Sh.Milioni 6.49 zikiwa ni malipo ya fidia ya Kiwanja namba 214 Kitalu G Kikuyu South Extension Dodoma kilichotwaliwa kwa ajili ya kupisha Mradi wa ujenzi wa Reli ya Mwendokasi.
……………………………………………………………………………………………………..
Na Alex Sonna, Dodoma
Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imewahukumu baba na mtoto kulipa faini Sh.Milioni 1.5 au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukiri kuahidi na kutoa rushwa ya Sh.Milioni 1.2 kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Dodoma, Sosthenes Kibwengo, amesema uamuzi wa shauri la jinai namba 148/2019 ulitolewa na mahakama hiyo kwa Mfanyabiashara Nahid Bahadur Hirji na mwanaye Bahadur Abdallah Hirji kwa kukiri mashtaka matatu ya rushwa yaliyokuwa yakiwakabili.
Amefafanua kuwa Mnamo Julai mwaka 2019, Takukuru iliwafikisha mahakamani hapo wafanyabiashara hao baada ya uchunguzi kuonyesha walifanya jinai hiyo kama kushawishi ili hatua stahiki zisichukuliwe dhidi yao kuhusiana na mgogoro wao wa kifamilia.
Amesema washtakiwa hao waliahidi na kutoa kiasi hicho cha fedha kwa Katambi kinyume na kifungu namba 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Hata hivyo, amesema pamoja na hukumu hiyo pia Mahakama hiyo imetaifisha Sh.Milioni 1.2 zilizokamatwa wakati wa mtego wa hongo hiyo.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU imewarejeshea fedha kiasi cha Sh.Milioni 28.97, wananchi wawili akiwemo Mwalimu Mstaafu Stanley Matonya ambaye pia ni Mkulima wa kijiji cha Itiso, wilayani Chamwino.
Kibwengo amesema Mwalimu huyo amerejeshewa Sh.Milioni 22.4 alizodhulumiwa na Kampuni ya Kabugama ya Jijini Dodoma tangu Agosti mwaka 2016.
“Mstaafu huyo aliingia mkataba wa kuuziwa trekta moja aina ya Swarrag 744 lenye jembe moja pamoja na tela kwa maelewano ya kulipa Sh.Milioni 23.98 ambayo ni asilimia 50 ya thamani ya trekta, pamoja na kulipa fedha hizo tangu Septemba 2016 Mwalimu huyo hakupata trekta na alipfuatilia aliambulia kurejeshewa Sh.Milioni 1.5,”amesema.
Kutokana na juhudi hizo kukwama, Mkuu huyo ameeleza kuwa Matonya alitoa taarifa TAKUKURU na uchunguzi umewezesha kampuni hiyo kurejesha kiasi cha Sh.Milioni 22.4 ambazo amekabidhiwa leo.
Aidha, amesema Taasisi hiyo imemrejeshea Mkazi wa Jiji la Dodoma Ahmed Talibu Sh.Milioni 6.49 zikiwa ni malipo ya fidia ya kiwanja namba 214 Kitalu G Kikuyu South Extension Jijini humo kilichotwaliwa kwa ajili ya kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi.
“Mei mwaka huu TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa Talibu kwamba ameshindwa kulipwa baada ya kuelezwa na Shirika la Reli linaloratibu zoezi hilo kuwa tayari malipo ya fidia ya kiwanja cha mwanaye Nasra Ahmed talibu yalishafanywa kwa mwananchi mwingine,”amesema.
Kibwengo amesema uchunguzi wa Taasisi hiyo ulibaini fidia hiyo imelipwa kwa Noorjan Adulhamid Ahmed baada ya kuwasilisha nyaraka alizozipata kwa njia ya udanganyifu na kufanikiwa kumrejeshea fedha hizo leo Ahmed kwa niaba ya mwanaye.
Pia, amesema Taasisi hiyo inaendelea kumtafuta mtuhumiwa aliyemuuzia kiwanja Noorjan na kumpatia nyaraka za kiwanja ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake.
Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya dhuluma ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya watu wanaofanya hivyo.