****************************************
WAGOMBEA ubunge saba wa vyama vya siasa vilivyokidhi masharti ya uteuzi na mawakala wao katika Jimbo la Ilemela wamekula kiapo kwa ajili ya kuingia kwenye chumba cha kuhesabia kura.
Wagombea hao walikula kiapo hicho jana mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela,John Wanga ili kuweza kupata fursa ya kuingia kwenye majumuisho ya kura za Rais, Wabunge na Madiwani kwa ngazi ya kata.
Akizungumza kabla ya kuwaapisha wagombea na mawakala hao Wanga alisema vyama 14 vilichukua fomu za kuwania ubunge lakini vyama 11 wagombea wake walirejesha fomu na kuvitaja kuwa ni CCM, ADC,ACT-Wazalendo, CUF,CHADEMA,DP, Demokrasia Makini na NRA.
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetekeleza shughuli mbalimbali kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani, uhuru na haki siku ya Oktoba 28 ambapo kampeni za uchaguzi huo zilizoanza Agosti 26, 2020 zitahitimishwa Oktoba 27, mwaka huu.
“Nitoe rai kwa wananchi,viongozi wa dini na wa vyama mbalimbali vya siasa pamoja na Watanzania wote wenye mapenzi mema kuitunza, kuilinda na kuienzi amani yetu kipindi chote kabla,siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi,”alisema Wanga.
Aidha alisema wananchi wa Jimbo la Ilemela waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura wajitokeze kwa wingi Oktoba 28, mwaka huu ambayo ni siku ya uchaguzi kuchagua viongozi (Rais, Wabunge na Madiwani) wanaowataka kwa ajili ya maendeleo yao ambapo vituo vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
Alieleza kuwa Jimbo hilo la Ilemela lina vituo 795 vya kupigia kura katika kata 19 na idadi ya wapiga kura 320,589 waliojiandisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ambapo majumuisho ya kura yatafanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela baada ya upigaji kura kukamilika.
Wanga alieleza zaidi kuwa katika jimbo hilo vifaa mbalimbali vya uchaguzi vinavyofikia asilimia 90 vimepokelewa kutoka NEC hadi sasa na hivyo uchaguzi utafanyika kwa ufanisi kadri ulivyopangwa.
Msimamizi huyo wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela alivionya vyama vya siasa ambavyo mawakala wao hawakuapishwa visithubutu kuwapeleka kwenye vituo vya uchaguzi kwani watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria sawa na wahalifu wengine isipokuwa walioapishwa.